TIMU ya Polisi Tanzania imetanguliza mguu mmoja kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kuwapiga maafande wa Magereza, Tanzania Prisons kwa mabao 4-0 ikijiweka sehemu nzuri ya kufuzu.

Mchezo huo wa mkondo wa kwanza wa mtoano  uliopigwa leo Julai 12, 2026 kwenye Uwanja wa Ushiriki mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Polisi ilionyesha nia yake ya kutaka kuimaliza mechi hiyo mapema ikiishambulia vikali Prisons.

Dakika ya 15, Polisi ikafanikiwa kupata bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti ikifungwa na Juhudi Philemon, akifungua milango ya ushindi kwa wanajeshi hao.

POLI 01

Penalti hiyo ilitokana na beki wa Prisons kuunawa mpira wakati akitaka kuzuia shuti la mshambuliaji Tariq Seif na mwamuzi Seleman Nonga kutoka Arusha hakusita kusimamia sheria 17 za soka.

Prisons dakika ya 27 ikapoteza nafasi nzuri, kichwa cha winga Haruna Chanongo, mpira ukagonga mwamba wa chini na kutoka nje akiunganisha kona ya Salum Kimenya.

Mpaka mapumziko Polisi ikatoka na uongozi wa bao 1-0 huku ikitawala mchezo huo wakati Prisons ikionekana kucheza kwa presha ikipambana kusawazisha.

POLI 02

Kipindi cha pili Polisi ikarudi na nguvu na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 46 likifungwa na Tariq kwa kichwa kizuri akimalizia krosi ndefu ya beki wa kulia na nahodha wa kikosi hicho, Denis Mushi.

Polisi ikaendelea kuwasakama Prisons na kufanikiwa kupata bao la tatu likifungwa na beki Tatizo Shem akifunga kirahisi akimalizia mpira uliotemwa na kipa Mussa Mbisa baada ya shuti la Mushi.

Emmanuel Mpuka akamalizia bao la nnne kwa mkwaju wa penalti dakika ya 73, akifunga kiufundi. Penalti hiyo ilitokana na Naku Kazimoto kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Nonga kutoa adhabu nyingine.

Timu hizo zitakutana kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Julai 16, 2026 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuamua timu ipi itacheza ligi kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *