Kulikuwa na hisia mchanganyiko wakati Simba ilipomtangaza Steve Barker kuwa Kocha wake Mkuu akichukua nafasi ya Dimitar Pantev ambaye iliachana naye.

Baadhi waliamini kwamba Barker ambaye kipindi hicho anajiunga Simba alitokea Stellenbosch ya Afrika Kusini, sio aina ya kocha ambaye angeiwezesha timu hiyo kupiga hatua kuendana na mahitaji yake hasa ya kufanya vizuri kimataifa.

Kile ambacho Stellenbosch ilikipitia siku kadhaa kabla ya Barker kutua Simba, kiliwapa wasiwasi kundi hilo na kulipa nguvu ya kuonyesha watu kuwa kocha huyo hatoweza kutimiza matarajio makubwa ya Simba.

Ikumbukwe wakati Barker anajiunga na Simba, aliiacha Stellenbosch ikiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini, ikiwa na pointi 12 ilizokusanya kwa kupata ushindi kwenye mechi tatu, sare tatu huku ikipoteza mechi nane.

Hata hivyo kuna kundi ambalo liliamini kwamba Barker ni aina ya kocha ambaye Simba imefanya uamuzi sahihi kumchukua.

Kuiongoza Stellenbosch kuingia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku ikiwa haijatumia kiasi kikubwa cha fedha katika kusuka kikosi chake kuliwapa tumaini kwamba akipewa nyenzo za kutosha na anazohitaji atawafikisha mbali.

Ilibakia suala la muda ili Barker aonyeshe upande upi ulikuwa sahihi katika fikra ambayo ilikuwa nao pindi alipojiunga na Simba.

Baada ya kuiongoza Simba kuanzia Januari hadi sasa Julai ambapo msimu wa 2025/2026 umemalizika, Barker amethibitisha kwamba wale walioamini timu hiyo imefanya uamuzi sahihi kumchukua walikuwa na mtazamo usio na shaka.

Kwa kuanzia, mapendekezo yake ya usajili katika dirisha dogo la usajili mengi yamekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya timu imalize msimu ikiwa na kiwango bora.

Anicet Oura, Libasse Gueye na Ismail Toure wamekuwa ni wachezaji walioongeza kitu kikubwa katika kikosi cha Simba kilichomaliza msimu kulinganisha na kile kilichoanza.

Oura amemaliza akiwa na mabao sita na pasi tatu za mwisho, Gueye akipachika mabao saba na kuchangia lingine moja huku Toure akiipa uimara zaidi safu ya ulinzi ya Simba.

Kocha huyo ameweza kutengeneza muunganiko mzuri wa kitimu. Simba imekuwa inajilinda na kushambulia vyema lakini pia imekuwa ikionyesha soka la kuvutia.

Barker pia ndani ya miezi saba aliyoiongoza Simba, amefanikiwa kufufua viwango vya wachezaji ambao walionekana kupoteza makali yao kabla ya ujio wake.

Mchezaji kama Elie Mpanzu ambaye mwanzoni mwa msimu alionekana kuporomoka kiwango hadi akatabiriwa kwamba atatupiwa virago na Simba, chini ya Barker amekuwa moto wa kuotea mbali tena akichezeshwa nafasi ya mshambuliaji wa kati ambayo sio yake kiasili.

Mfano mwingine ni beki David Kameta ‘Duchu’ ambaye baada ya kusotea benchi kwa muda mrefu, chini ya kocha huyo tumeshuhudia akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Chini ya Barker, Simba imeondoa unyonge ambao ilikuwa nao katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya washindani wake wakuu, Yanga na Azam FC.

Tangu aanze kuinoa Simba, Barker hajapoteza mechi nne ambazo timu yake imecheza dhidi ya Azam na Yanga katika mashindano tofauti ambapo Simba imepata ushindi mara mbili na kutoka sare mbili.

Kubwa zaidi, Barker ameifanya Simba imalize msimu kibabe kwa kuiongoza kutwaa mataji mawili kwa kuwafunga wapinzani wake wakuu katika fainali.

Simba ilitwaa Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga bao 1-0 katika fainali na ikapata ushindi kama huo katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Azam FC.

Taji la Kombe la Shirikisho la CRDB limechukuliwa na Simba baada ya timu hiyo kukaa miaka mitano bila kulitwaa tangu ilipolichukua mwaka 2021.

Katika Ligi Kuu ya NBC, japo Simba haikufanikiwa kutwaa ubingwa katika msimu uliomalizika, safari hii imemaliza ikiwa na pengo dogo la pointi baina yake na Yanga tofauti na misimu minne iliyopita ambayo sio tu ilikosa ubingwa bali pia iliachwa kwa tofauti kubwa ya pointi.

Msimu wa 2024/2025, Simba iliachwa kwa pointi tano na Yanga, msimu wa 2023/2024 ilizidiwa kwa pointi 11, ikazidiwa pointi tano katika msimu wa 2022/2023 na katika msimu wa 2021/2022, Yanga iliwaacha kwa pointi 13.

Aina ya makocha kama Steve Barker ndio tunaohitaji kuwaona wakija katika Ligi yetu wakitokea nje ya nchi.

Makocha ambao wanaleta mabadiliko chanya katika timu zetu lakini pia wanakuwa darasa kwa makocha wetu wazawa katika namna ya kuzisimamia timu kimbinu, kiufundi na hata kiutawala wa wachezaji.

Soka letu halihitaji makocha wa kigeni ambao wanakuja nchini kujifunzia kwetu. Fursa kama hiyo ni kwa ajili ya makocha wazawa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *