Dar es Salaam. Msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amemtaja mrithi wa mali zake zote, huku kauli hiyo akiitoa kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mama yake mzazi, Sanura Kassim.

Katika sherehe hiyo ya kutimiza miaka 59 ya mama yake, Diamond alimkabidhi zawadi zenye thamani kubwa ikiwemo saa aina ya Rolex yenye thamani ya takribani Sh166 milioni pamoja na seti ya dhahabu iliyokuwa na cheni na bangili Pamoja na hereni.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Diamond amesema hataki kupindisha maelezo kuhusu suala la urithi wa mali zake na mama yake ndiye mtu muhimu zaidi kwake na ndiye anayestahili kuwa na kila alichonacho.

“Sitaki kupindisha maelezo, nyumba tunayokaa ni ya mama yangu, mali zangu zote ni zake. Cha kwangu ni cha mama yangu, kwa hiyo haiwezi ikatokea huko mtu akasema kuna mtu mwingine anarithi,” amesema Diamond.

Diamond alieleza mafanikio aliyoyapata yamekuwa na nafasi kubwa ya mama yake, hivyo anaona ni jambo la msingi kuhakikisha mama yake anakuwa na kila kitu anachostahili.

Kauli hiyo ya Diamond imeonyesha kumuenzi mama yake na kuonyesha wazi nafasi yake katika maisha yake pamoja na mafanikio yake.

Kwa miaka mingi, Diamond amekuwa akieleza kuhusu umuhimu wa mama yake katika safari yake ya muziki, huku Bi Sanura akiwa mmoja wa watu waliokuwa karibu naye tangu mwanzo wa safari yake ya mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *