IRINGA: Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Ng’uruhe pamoja na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilolo, ikisema miradi hiyo inaonyesha utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya elimu.

Kamati hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, ilikagua miradi hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama na kujionea namna fedha za umma zinavyotumika kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Yasin alisema wajumbe wa kamati wameridhishwa na ubora wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa wananchi wana wajibu wa kuitunza ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu kwa kujenga shule mpya, mabweni, maabara na vyuo vya ufundi, hatua inayopanua fursa za elimu na kuwawezesha vijana kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

“Tuko katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Chama ndicho kinachosimamia Serikali, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha miradi inayotekelezwa inawanufaisha wananchi. Tumeridhishwa na maendeleo ya miradi hii na tunaamini italeta mabadiliko makubwa kwa jamii,” alisema Yasin.
Katika Shule ya Sekondari Ng’uruhe, kamati ilielezwa kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 200 kujenga shule hiyo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Makwema na kusogeza huduma ya elimu karibu na wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema ujenzi wa shule hiyo umeondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata masomo na ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya kujifunzia katika halmashauri zote za mkoa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Makwema, Newas Mtenga, Shule ya Sekondari Ng’uruhe yenye namba ya usajili S.8667 tayari imeanza kutoa huduma ikiwa na walimu watano na wanafunzi 68 waliohamishwa kutoka Shule ya Sekondari Makwema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’uruhe, Martin Kifiyasi, alisema shule hiyo imeondoa msongamano uliokuwa umeikumba Shule ya Sekondari Makwema iliyokuwa na zaidi ya wanafunzi 600, huku mwananchi Merina Kisoma akisema wazazi wamepunguziwa gharama za usafiri na wanafunzi hawalazimiki tena kutembea umbali mrefu, jambo lililosaidia kupunguza utoro.

Kamati hiyo pia ilikagua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilolo kinachojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.6 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Afisa Udhibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Kilolo, Alto Kinunda, hadi Julai 9 mwaka huu Serikali ilikuwa imepeleka Sh Milioni 777.4 kwa ajili ya mradi huo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 608 zimetumika na ujenzi umefikia asilimia 76.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo tisa, yakiwemo jengo la utawala, madarasa matatu, karakana za useremala, uashi, umeme na ufundi bomba, ushonaji na upishi, jengo la umeme, nyumba ya mtumishi, jengo la mlinzi pamoja na vyoo vya jumuiya.
Kinunda alisema chuo hicho kinatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2026 na kitapokea wanafunzi wapatao 240 katika fani mbalimbali za ufundi.
Alisema uwepo wa chuo hicho utawapa vijana wa Wilaya ya Kilolo na maeneo jirani fursa ya kupata ujuzi wa kazi, kuongeza ajira na kujiajiri, hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.