BAADA ya Kagera Sugar kurejea Ligi Kuu Bara, imeendelea kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji mbalimbali kati ya hao ni Dickson Mhilu aliyesaini mkataba wa miaka miwili hadi 2028.

Msimu ulioisha, Mhilu ameichezea Dodoma Jiji iliyomaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 35, nyota huyo  baada ya kumaliza mkataba wake akaamua kurejea Kagera inayonolewa na kocha Juma Kaseja.

Rafiki wa karibu na mchezaji huyo, amesema Dickson aliona arejee kuongeza nguvu katika timu iliyochangia kukuza kipaji chake na aliipiga chini ofa mpya ya Dodoma. “Alianza kufanya mazungumzo na Kagera mara baada ya kupanda Ligi Kuu, hivyo ikawa rahisi kwake kukubaliana na ofa hiyo na anaona ni timu ya nyumbani,” amesema rafiki yake huyo.

Alipotafutwa kaka yake na Dickson ambaye ni Yusuf Mhilu aliyeipandisha daraja Geita Gold, amesema anachojua mdogo wake amerejea Kagera, ingawa hawezi kuelezea kiundani zaidi.

“Nadhani amesharejea Kagera, lakini sina taarifa zake zaidi kumuhusu kwani msimu ulipomalizika kila mtu alipata nafasi ya kupumzika na kutenga muda wa kujua anaenda wapi,” amesema.

Mhilu anayecheza beki wa kulia, amewahi kucheza Kagera Sugar kabla ya kutimkia Tanzania Prisons na baadaye Dodoma Jiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *