LILE lililoonekana kama dili la uhakika la beki wa kati wa TRA United, Nasri Kombo kutua Yanga, taarifa zinabainisha kwamba limegonga ukuta baada ya nyota huyo kufanya uamuzi wa kubaki klabuni hapo na kusaini mkataba mpya wa miaka miwili.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hatua hiyo imeizima uhamisho wake wa kutua Yanga katika dirisha hili la usajili huku TRA United ikifanikiwa kumbakisha mmoja wa wachezaji wake muhimu waliochangia uimara wa safu ya ulinzi msimu uliopita.

Kwa muda mrefu, beki huyo alikuwa kwenye orodha ya wachezaji waliokuwa wakifuatiliwa na Yanga iliyokuwa ikisaka beki wa kati mzawa wa kuongeza ushindani kwenye kikosi hicho kuelekea msimu mpya.

KOMB 01

Mpango wa mabingwa hao ulikuwa ni kuongeza nguvu katika nafasi hiyo ili kushirikiana na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Bakari Mwanyeto na Dickson Job, hasa baada ya kuamua kuachana na beki raia wa Ghana, Frank Assinki aliyekuwa akicheza hapo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.

Vigogo hao wa Jangwani walipanga kutumia nafasi ya beki mzawa ili kuacha nafasi zaidi kwa usajili wa wachezaji wa kigeni kwenye maeneo mengine yanayohitaji kuongezewa nguvu, jambo lililomfanya Scoba kuwa mmoja wa chaguo lao la kwanza.

Hata hivyo, TRA United haikuwa tayari kumpoteza kirahisi beki huyo ambaye amekuwa mmoja wa viongozi ndani ya kikosi, ikamuwekea mezani mkataba mpya ambao ameukubali na kuamua kuendelea na maisha yake ndani ya timu hiyo.

Uamuzi huo unatajwa kuwa ni ushindi kwa TRA United ambayo inajipanga kujenga kikosi imara zaidi ya baada ya kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya tano ya Ligi Kuu.

KOMB 02

Carlos Sylvester ‘Mastermind’ ambaye anamsimamia beki huyo, akizungumzia mustakabali wa Kombo ndani ya TRA, amesema: “Tuwashukuru sana TRA, mwalimu wao na benchi zima la ufundi sambamba na viongozi wameweza kumpa nafasi ambayo inamfanya sasa watu kumuongelea kwa namna yao wanavyotaka kutafsiri.

“Mkataba wake na TRA umekwisha baada ya msimu kumalizika, hivyo ni mchezaji huru, lakini nafasi kubwa tunawapa TRA ya kumuongezea mkataba kwa sababu bado wanamuhitaji, tunaheshimu kutokana na nafasi waliyompa na mimi naona ndio mahusiano mazuri kwamba wameishi naye vizuri muda wote, ukiniuliza tukisema tunachagua timu tatu ya kwenda, basi ya kwanza ni TRA.”

Baada ya mlango wa Kombo kufungwa, Yanga haijapoteza muda na sasa imehamishia nguvu zake kwa beki wa kati wa Mashujaa FC, Mohamed Mussa ambaye ameonekana kuwa chaguo linalofuata katika mpango wa kuimarisha safu ya ulinzi.

Taarifa zinaeleza kuwa, mazungumzo kati ya Yanga na Mashujaa yamefikia hatua nzuri huku pande hizo zikikubaliana kuhusu ada ya uhamisho wa mchezaji huyo.

Kinachosubiriwa kwa sasa ni Yanga kukamilisha dili hilo ni upande wa malipo kwa kuingiza fedha kwenye akaunti ya Mashujaa kabla ya taratibu za mwisho za usajili kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *