
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa mkataba wa maelewano (MoU) uliosainiwa hivi karibuni baina yake na Marekani sasa uko katika hali ya mkwamo, kufuatia hatua ya Washington kukiuka ahadi zake. Mkatataba huo unajulikana kama Mkataba wa Islamabad kutokana na kuhusika Pakistan katika jitihada za upatanishi baina ya pande hizo mbili.
Aidha, Iran imebainisha kuwa mazungumzo kuhusu utaratibu wa usalama wa njia ya baharini katika Lango la Hormuz yamegonga mwamba kutokana na shinikizo la Marekani dhidi ya taifa la Oman.
Akizungumza katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, ameonya vikali kuwa eneo lolote litakalotumiwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran litakabiliwa na jibu mwafaka.
Amesema: “Iran haijawahi kuwa ya kwanza kukiuka wajibu wake. Iran imekuwa ikishiriki katika kila mazungumzo kwa umakini, kwa nia njema, na kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa. Upande uliovunja ahadi zake ni Marekani.”
Ameongeza kuwa Washington haikusubiri hata kipindi cha mwezi mmoja kilichotajwa katika Kifungu cha Tano kuhusu Lango la Hormuz kumalizika, kabla ya kuanza kukiuka ahadi zake.
Mnamo tarehe 17 Juni, Iran na Marekani zilisaini mkataba huo wa maelewano ambao unatoa wito wa kusitishwa kikamilifu kwa uhasama katika nyanja zote, na unajumuisha ahadi kutoka pande zote mbili kufanya mazungumzo zaidi kuelekea mkataba wa mwisho ndani ya siku 60. Kifungu cha 5 kinakabidhi wajibu wa kufungua na kusimamia Lango la Hormuz mikononi mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baghaei amesisitiza kuwa mazungumzo yaliyofanyika Jumamosi mjini Muscat baina ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Oman yalilenga suala la Lango la Hormuz pekee, na hakukuwa na majadiliano yoyote kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Amesema kutokana na shinikizo lililowekwa dhidi ya Oman, mkutano huo wa Muscat haukuwa na mafanikio.
Kuhusu usalama wa kikanda, Baghaei amesisitiza kuwa Iran haijashambulia na haina nia ya kushambulia nchi yoyote katika kanda hii.
Ameema kuwa Iran imezitaka mara kwa mara nchi za kanda hii zisiruhusu Marekani na utawala haramu wa Israel kuzitumia nchi zao kama uwanja wa mashambulizi dhidi ya Iran, akielezea hilo kama kanuni ya sheria za kimataifa na wajibu wa kimaadili na kisiasa.
Baghaei pia amesisitiza kuwa kulipiza “kisasi cha damu” kwa ajili ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ni takwa la taifa zima la Iran. Amesisitiza kuwa Iran itatumia mifumo yote ya kisheria ya kimataifa na ya ndani ili kuhakikisha wale waliohusika wanawajibishwa.
Ayatullah Khamenei aliuawa shahidi, pamoja na baadhi ya wanafamilia yake, mnamo tarehe 28 Februari, siku ya kwanza ya vita haramu vya kigaidi vya siku 40 vilivyozinduliwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.