Wakati wengi wakiamini waamuzi kutoka Ufaransa, François Letexier na Clément Turpin wameondolewa kuchezesha Kombe la Dunia 2026 kutokana na utata wa mchezo kati ya Argentina na Misri, ukweli ni kwamba hatua hiyo ni sehemu ya kanuni za muda mrefu za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), zinazowazuia waamuzi kutoka mataifa yaliyofuzu nusu fainali kuendelea kuchezesha mechi za hatua za mwisho.

Mwamuzi pekee kutoka Ufaransa aliyebaki kwenye orodha ya FIFA ni Jérôme Brisard, ambaye ameendelea kutekeleza majukumu yake kama mwamuzi wa teknolojia ya VAR.

Waamuzi hao walijikuta katikati ya mjadala baada ya Argentina kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Misri katika mchezo wa 16 bora uliokuwa na matukio ya utata.

Katika mchezo huo, Misri ilikataliwa bao katika kipindi cha pili baada ya VAR kubaini kuwa Marwan Attia alimfanyia faulo Lisandro Martínez kabla ya Mostafa Zico kufunga.

Mbali na hilo, wachezaji wa Misri walidai walistahili kupewa penalti baada ya Mohamed Salah kuangushwa ndani ya eneo la hatari muda mfupi kabla ya Argentina kufunga bao la ushindi katika dakika za nyongeza.

Baada ya mchezo huo, Shirikisho la Soka la Misri (EFA) liliwasilisha malalamiko rasmi kwa FIFA likitaka uchunguzi ufanyike dhidi ya Letexier pamoja na timu yake ya waamuzi. Kocha wa Misri, Hossam Hassan, pia aliwashutumu waamuzi hao kwa madai ya kuibeba Argentina na kumsaidia Lionel Messi kuelekea fainali.

Hata hivyo, FIFA haijachukua uamuzi huo kama adhabu dhidi ya waamuzi hao badala yake, hatua hiyo inatokana na kanuni za muda mrefu za shirikisho hilo zinazozuia waamuzi kutoka mataifa yaliyofuzu hatua ya nusu fainali kuendelea kuchezesha mechi zilizobaki ili kuepusha mgongano wa maslahi.

Kutokana na Ufaransa kufuzu hatua ya nusu fainali, waamuzi wake hawakuwa na nafasi ya kuendelea kupewa mechi za hatua za mwisho.

Kanuni hiyo pia imewaathiri waamuzi kutoka mataifa mengine yaliyofuzu nusu fainali, ikiwemo Argentina, Hispania na England.

FIFA inaamini utaratibu huo unasaidia kulinda uadilifu wa mashindano na kupunguza mjadala kuhusu maamuzi ya waamuzi katika hatua muhimu za kuwania ubingwa, huku ikitaka mechi zilizosalia ziamuliwe na uwezo wa wachezaji badala ya mjadala wa uamuzi wa waamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *