Arusha. Vyuo vikuu sita vilivyo Kusini mwa Jangwa la Sahara vitanufaika na mradi wa kuboresha taaluma kwa wanafunzi na wafanyakazi kwenye maeneo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, teknolojia za matumizi bora ya nishati na ubunifu wa kidijitali ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi.

Mradi huo wa miaka minne unaotekelezwa kwa pamoja na kusimamiwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) unafadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) itakayotoa jumla ya Sh4 bilioni.

Akizindua mradi huo leo Jumanne, Julai 14, 2026, Naibu Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Profesa Anthony Mshandete amesema mradi huo wa kikanda utazinufaisha nchi za Tanzania, Malawi, Ivory Coast, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Chuo Kikuu cha Genk, Ubelgiji.

“Pamoja na mambo mengine, lengo kuu la huu mradi ni kubadilishana maarifa ya kitaaluma kwenye mambo makuu matatu ambayo ni mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta ya kilimo, teknolojia za nishati jadidifu na uchumi wa kidijitali ambayo ni mahsusi kwa sababu yanalenga kutatua changamoto zilizopo barani Afrika,” amesema Profesa Mshandete.

Amesema mradi huo utasaidia kuviunganisha vyuo vikuu ambavyo vipo kwenye mradi kuja na teknolojia zilizozalishwa barani Afrika kwa ajili ya kutatua changamoto hizo kupitia wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo na wafanyakazi ambao ni walimu wanaofundisha kwenye nyanja husika.

Profesa Mshandete ameongeza kuwa mradi huo unaenda kuchagiza utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuja na teknolojia za kilimo zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, teknolojia za nishati jadidifu na teknolojia zitakazoboresha uchumi wa kidijitali.

Mratibu wa mradi huo, Profesa Linus Munishi amesema unafadhiliwa chini ya mpango wa uhamaji wa kitaaluma wa ndani ya Afrika wa Umoja wa Ulaya ukiwa umeundwa ili kuimarisha vyuo vikuu vya Kusini mwa Sahara.

“Mradi huu unatoa ufadhili kamili wa masomo ya shahada ya uzamili na uzamivu kwa wanafunzi kusoma katika mataifa mbalimbali ya Afrika yanayoshiriki na unajenga ujuzi katika kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, teknolojia za matumizi bora ya nishati na ubunifu wa kidijitali,” amesema Profesa Munishi.

Amesema mpango huo unawezesha uhamaji wa kimfumo, ukiwaruhusu wanafunzi wa ngazi ya uzamili, watafiti na wafanyakazi kusoma na kufanya utafiti katika vyuo vikuu washirika wakilipiwa ada yote ya masomo huku mpango ukisisitiza ushiriki wa wanawake usipungue asilimia 25.

Ofisa Progamu kutoka Umoja wa Ulaya hapa nchini na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Alessandro Pisani amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza wataalamu kwenye nyanja zilizoanishwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara la Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *