Chanzo cha picha, Getty images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Siku ya Jumatatu asubuhi, katika chapisho kupitia mitandao ya kijamii Donald Trump alitangaza Marekani itaanza tena kuzizuia meli za Iran, pia alisema meli zote zinazopitia Mlango-Bahari wa Hormuz – ikiwa ni pamoja na zile za washirika wa Marekani – lazima zilipe ada ya 20% ili kuilipa Marekani “gharama zinazohitajika ili kufanya kazi ya kutoa usalama” katika mlango wa huo wa bahari.
Siku iliyofuata, aliachana kabisa na pendekezo hilo, badala yake ameahidi ataingia katika “mikataba ya kibiashara na uwekezaji” na washirika wa Marekani wa Ghuba.
Mabadiliko hayo ya ghafla ni ya hivi punde katika mzozo ambao sasa umedumu kwa zaidi ya miezi minne, na licha ya “mkataba wa makubaliano” wa mwezi mmoja uliohakikisha kusitishwa mapigano kwa muda na kuweka mfumo wa mazungumzo zaidi, hauonyeshi dalili zozote za kumalizika.
Huenda Trump akasita kuzidisha makali ya vita kutokana na vita hivyo kutopendwa, uwezekano wa kupanda kwa bei za nishati na hatari kwa vikosi vya Marekani na washirika wa Marekani kushambuliwa tena na Iran.
Na kumaliza mgogoro huo bila kufikia makubaliano ambayo anaweza kudai ni bora kuliko yale ambayo utawala wa Barack Obama uliyapata mwaka 2015, pia ni jambo asilolitaka.
Rosemary Kelanid, Mkurugenzi wa Masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Defense Priorites anasema, “Hivi ni vita vya kuchoshana, na vita vya kuchoshana huendelea kwa muda mrefu sana.”
Mkataba wa makubaliano kati ya Marekani na Iran (MOU) – na matumaini ya kukomesha vita – yalikufa siku ya Jumanne kwenye Truth Social, wakati Trump alipotangaza kuanza tena kwa vizuizi vya Marekani dhidi ya meli za Iran, huku kukiwa na mashambulizi mengi ya kijeshi ya Marekani kote Iran.
Iran ilijibu kwa kufanya mashambulizi dhidi ya washirika wa Marekani na meli za kibiashara katika eneo hilo, na kuvuruga safari katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mgogoro haujatatuliwa
Baada ya karibu mwezi mmoja wa mazungumzo ya kwenda na kurudi ya kusitisha mapigano, kati ya mataifa hayo mawili, yenye uhasama, Trump na Wamarekani wanaonekana kukabiliwa na changamoto zile zile zilizokuwepo kabla ya Vita na Iran.
Ingawa kijeshi, Marekani imefanikiwa katika malengo yake, kama vile kuharibu meli za Iran, ndege na uwezo wa ulinzi kudhoofika, kisiasa mgogoro huo bado haujatatuliwa.
Ingawa Iran imedhoofika kijeshi, bado ina uwezo wa kuvuruga shughuli za Mlango-Bahari wa Hormuz. Na Marekani ina uwezo mdogo wa kuizuia.
Mwezi uliopita tu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alilaani mpango wa Iran wa kutoza “ushuru” kwa meli zinazopita Hormuz.
“Hakuna nchi inayoruhusiwa kutoza ushuru au ada kwenye njia ya maji ya kimataifa,” alisema. “Hiyo ndiyo sheria ya kimataifa iliyopo. Hivyo ndivyo ilivyo katika njia za maji za kimataifa kote ulimwenguni, na hivyo ndivyo tunavyotarajia hapa.”
Trump kuachana na mpango wa kutoza ushuru wa 20% kwa meli zinazopita Hormuz ni ushahidi kwamba rais huyo anaonekana kutokuwa na njia iliyo wazi ya kusonga mbele.
Mkataba wa makubaliano, ambao Wamarekani na Wairani walidai kuwa ni ushindi kwa upande wao, haukuwa wazi kwenye mambo mengi, na uliacha mambo mengi yaingizwe katika mazungumzo ya baadaye.
Hati hiyo ilitoa jukumu fulani kwa Iran kusimamia upitaji salama wa wa meli huko Hormuz. MOU pia ilijumuisha mabilioni ya dola katika “uwekezaji” ulioahidiwa kwa Iran na kukomeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran.
Huenda Marekani iliamini uzuri wa ahadi hizo, zilizoambatana na maonyo kuhusu athari ikiwa Iran haitotii, yangetosha kuizuia Iran kujaribu kutumia nguvu zake za kijiografia kudhibiti mlango bahari wa Hormuz. Hesabu hiyo kwa sasa, inaonekana si sahihi.
“MOU imekufa kabisa,” anasema Kelanid. “Mambo yote yaliyoainishwa sasa yamefutwa.”
Sasa Trump, na Iran, wanajikuta katika hali ngumu. Iran inakabiliwa na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani katika eneo lao, haina uwezo wa kujilinda. Na kwa kizuizi kilichowekwa tena, mapato yao ya mafuta – ambayo ni muhimu kwa utawala wa Iran – yamekatwa tena.
Wakati huo huo, Trump anakabiliwa na chaguo kati ya kuongeza makali ya vita, jambo ambalo litasababisha gharama za kiuchumi na kisiasa ndani ya Marekani, huku akiuacha utawala wa Irani madarakani.
“Tumerudi mahali tulipokuwa mwanzoni, ambapo swali lilikuwa: ni nani mwenye subira zaidi?” anasema Elliot Abrams, mtafiti mwandamizi wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya fikra tunduizi ya Council on Foreign Relations.
“Iran, ambayo haitaweza kusafirisha mafuta nje, au Marekani na nchi zingine zinazotumia mafuta ya ghuba ya Uajemi?”
Trump njia panda
Chanzo cha picha, Reuters
Baada ya miezi kadhaa ya wasiwasi kwamba vita vya Iran vinasababisha kuporomoka kwa umaarufu wa Trump na mfumuko wa bei, Trump alipokea habari njema Jumanne kwamba bei zimeanza kushuka.
Kuanza tena kwa mashambulizi, bila shaka kutaisukuma bei ya mafuta kupanda na kurudi katika viwango vya juu vya awali, na kuwaweka Warepublican katika nafasi dhaifu kuelekea uchaguzi wa bunge wa Novemba.
Siku ya Jumatatu, baada ya chapisho la Trump, bei ya pipa la mafuta ilipanda karibu 10% – ongezeko kubwa zaidi la siku moja katika miaka sita.
Mara ya kwanza, vikwazo vya Trump vilisaidia kuishinikiza Iran kwenda kwenye meza ya mazungumzo, lakini sasa kulingana na Kelanid, nguvu za Trump juu ya Iran huenda zikapungua.
“Tayari amefanya mambo ambayo anaweza kuyafanya kwa urahisi,” anasema. “Anaweza kushambulia maeneo ya kijeshi, maeneo ya serikali. Amefanya hivyo hapo awali, na haikusababisha Iran kujisalimisha.”
Ikiwa hatua za hivi karibuni za Trump hatimaye zitasaidia kuleta mazungumzo mengine ya kusitisha mapigano, mivutano ya msingi kuhusu Hormuz, kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kuhusu ushawishi wa Iran katika Mashariki ya Kati – bado itabaki.
Huku vita vikikaribia mwezi wake wa tano, Trump Jumatatu alibainisha kuwa migogoro mingine ya Marekani – ikiwa ni pamoja na Vita vya Vietnam – viliendelea kwa miaka mingi.
Hata hivyo, vita hivyo vilimaliza urais wa Lyndon Baines Johnson na kuharibu hadhi ya Marekani duniani.
Huku makubaliano yakivunjika, usitishaji mapigano ukiisha na uwezekano wa mzozo zaidi ukikaribia, mwisho wa Vita vya Iran hauonekani kuwa karibu.