
UONGOZI wa Mashujaa FC, umefungua mazungumzo na beki wa Mtibwa Sugar, Haroun Lyawatwa baada ya Azam na Singida Black Stars zilizokuwa zinafuatilia huduma ya nyota huyo tangu mwanzoni kuonyesha dalili za kutoendelea naye.
Mashujaa inamfuatilia beki huyo baada ya Mohamed Mussa kudaiwa anakaribia kujiunga na Yanga, iliyoingia kuiwinda saini yake kufuatia chaguo la kwanza ambalo ni la nahodha wa TRA United, Nasri Kombo kuamua kubakia na kuongeza mkataba mpya.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Mashujaa, umeliambia Mwanaspoti tayari beki huyo wamefikia makubaliano ya kujiunga na kikosi hicho kwa mkataba wa miaka miwili, japo kilichobaki ni kumuingizia kwanza fedha za usajili.
“Kila kitu kimekamilika baada ya mazungumzo chanya kufanyika kati ya pande zote mbili, kilichobakia ni kusaini mkataba na hilo litakamilika hivi karibuni tutakapoingiza fedha zake za usajili tulizokubaliana awali,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika, amesema wameshapokea ripoti ya benchi la ufundi kwa ajili ya kufanyia maboresho mbalimbali katika kikosi hicho cha maafande, ingawa hadi sasa hakuna usajili uliokamilika.
“Mchakato umeanza lakini hakuna makubaliano tuliyofikia na mchezaji yeyote kwa sababu tulikuwa tunahitaji tupokee ripoti ya benchi la ufundi, muda ukifika kila kitu tutaweka wazi ili mashabiki zetu waone wachezaji wao wapya,” amesema Tika.
Licha ya Mtibwa Sugar kushuka daraja hadi Championship, ila Lyawatwa alikuwa beki bora wa kikosi hicho, alikifungia pia bao moja katika sare 2-2 dhidi ya JKT Tanzania, Mei 24, 2026.