
ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga na Azam FC, Prince Dube amesema ushindani wa Ligi ya Tanzania aliyoushuhudia kwa kipindi alichocheza takribani miaka sita, umemjenga na kuacha heshima ya kumbukumbu katika kazi yake ya mpira wa miguu.
Azam ndiyo ilikuwa timu ya kwanza kwa mshambuliaji huyo kuichezea hapa nchini kuanzia 2020 hadi 2024 akitokea Highlanders ya kwao Zimbabwe, baadaye akasajiliwa Yanga alipodumu misimu miwili 2024-2025 na 2025-2026, kisha hivi karibuni amerejea nchini kwao Zimbabwe na kutua Hardrock.
Dube amesema Ligi Kuu Bara imempa chalenji nzuri ya ushindani, akiamini licha ya kuondoka itazidi kuwa bora na msimu unaokuja utakuwa mgumu na wenye mapambano makali.
“Ligi ya Tanzania ina chalenji nzuri, naamini kila mchezaji anafurahia kucheza, binafsi nilifurahia kwa kipindi nilichokuwa nacheza,” amesema Dube na kuongeza;
“Nitazikumbuka timu zote nilizochezea kwa nyakati tofauti, kuondoka kwangu nilihitaji changamoto mpya ya ushindani, lakini sitaacha kuikumbuka ligi hiyo kuwa kati ya ligi bora kwangu.”
Takwimu za Dube katika Ligi Kuu Bara zipo hivi; Akiwa Azam msimu wa 2020-2021, alifunga mabao 14, huku 2021-2022 aliingia kambini mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha ambayo yalimuweka nje, kisha 2022-2023 alifunga mabao 12 na 2023-2024 alikuwa na mabao saba.
Pale Yanga, msimu wa 2024-2025 alimaliza na mabao 13 na 2025-2026 akamaliza na mabao 10.