ALIYEKUWA Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emanuel Kimbe, amesema uongozi wa timu hiyo unapaswa kuzingatia ripoti ya benchi la ufundi kuhakikisha makosa yaliyofanyika msimu wa 2025-2026 yasijirudie.
Mbeya City haikuwa na matokeo mazuri katika Ligi Kuu msimu huo ilipomaliza nafasi ya 14 kwa pointi 30 na kuangukia mtoano ‘Play Off’ ilipofanikiwa kushinda kwa jumla ya mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Kimbe anakumbukwa kuiongoza timu hiyo kwa takribani miaka 12 ikiwa na mafanikio ya kucheza Ligi Kuu bila kushuka daraja kabla ya kukutwa na aibu hiyo msimu wa 2022-2023 na kutangaza kuachia nafasi hiyo.
Mafanikio zaidi kwa kigogo huyo ni kuiweka nafasi ya tatu kwa mara ya kwanza walipopanda Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 kisha nafasi ya nne msimu uliofuata, historia ambayo haijafikiwa kwa viongozi wengine.
Hata hivyo, katika mchezo wa mwisho wa play off dhidi ya Prisons, mashabiki wa timu hiyo walisikika jukwaani wakiimba jina la Kimbe, hali iliyovuta hisia kuwa huenda akarejea kikosini kuanzia msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kimbe amesema lazima wafanye maandalizi ya mapema na kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi ndio inaweza kuwa suluhisho kwa timu hiyo kufanya vizuri.
“Wazingatie mapendekezo ya kocha kwakuwa ni mzoefu na mwenye uwezo, wasirudie makosa hadi kuweka presha, tulisaidia wengi dakika za mwisho kutokana na mapenzi yetu,” amesema Kimbe.
Kuhusu hatma yake ya kurejea kikosini, kigogo huyo amesema hajawa na mpango wa kurejea kwenye timu kwani hajaamua kurudi kwenye mpira kutokana na majukumu aliyonayo nje ya soka.
“Wakati naondoka kwenye timu niliachia kwa mapenzi yangu, hivyo kurejea kwangu tena itategemeana na vipengele, mchango wangu katika mechi za mwishoni msimu uliopita ilikuwa ni uamuzi wangu na tulikuwa wengi,” amesema kigogo huyo.