Waandishi wa habari wamepewa jukumu jipya la kuhamasisha jamii juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kusukuma adhma ya Serikali asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Ni mafunzo maalum kwa waandishi wa habari, maafisa mawasiliano na maafisa habari yanayoendelea Mkoani Morogoro.
Lengo ni kubadili namna taarifa za nishati safi zinavyowasilishwa kwa jamii.

Akifungua mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kubadilisha fikra za wananchi.

“Waandishi tuambieni jamii faida za nishati safi. Tueleze fursa zilizopo hasa kwa wanawake na vijana,Nishati safi inatoa ajira, inapunguza magonjwa na inalinda misitu yetu.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolascos Mlay amesema mafunzo haya yanalenga kupata kauli moja kitaifa.

“Tunataka sote tuzungumze lugha moja. Jamii ipate taarifa sahihi ili ichague nishati inayolingana na uwezo wake.”

Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji, UNCDF, Emanuel Muro naye ameeleza mkakati wa shirika hilo.

“Sisi tunahakikisha tunatoa suluhisho ambalo mwananchi anaweza kumudu gharama yake. Si lazima iwe ghali. Tunataka nishati safi iwe kwa kila mtu.”

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Muda Kilakala amesema elimu zaidi inahitajika vijijini ambako ndiko chanzo kikuu cha uzalishaji wa mkaa na kuni.

“Kazi yetu sasa ni kutoa elimu vijijini. Tuwafundishe wananchi faida za nishati safi ili tuweze kufikia lengo la Serikali.”

Jitihada hizi ni sehemu ya azma ya Serikali kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo 2034.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *