
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitaendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na wanachama wanaokiuka kanuni za chama hicho ikiwamo kupeleka malalamiko kwenye vyombo vya habari badala ya kutumia vikao halali.
Kauli hiyo ya msisitizo imekuja wakati kukiwa na mfululizo wa baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho, wanaojitokeza hadharani kutaka uchunguzi na hatua za kinidhamu zilichukuliwe dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche.
Tayari, viongozi takribani sita wanaotoka mikoa ya Tanga, Morogoro na Dodoma wamepewa barua ya kutoa ushahidi wa tuhuma wanazozitoa dhidi ya Heche ndani ya siku 14.
Hata hivyo, Julai 10, 2026 akisoma maazimio ya kamati kuu iliyoketi kuanzia Juni 28 hadi 30 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema fedha zote zinazochangwa zipo salama na zinatumika kwa mujibu taratibu za chama za kifedha kwa uamuzi wa vikao.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Julai 15, 2026, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Nshala Rugemeleza amesema viongozi au makada wanaofanya hivyo hawana tofauti na wasaliti dhidi ya chama hicho.
“Wanaokubali kuingia katika mfumo watachukuliwa hatua, waache waseme maneno yao machafu lakini hatua za kinidhamu zitafanywa na zinafanywa dhidi yao. Chama hakitawasahau usaliti na uasi wao na tutachukua hatua zinazostahiki.
“Watu waovu hatuwezi kuwasamehe, kwa sababu wanakisaliti chama anastahili adhabu ya kutoka hatuwezi kukaa na wasaliti watakaoshughulikiwa kwa mujibu wa chama chetu, kwa wakati unastahili watapata adhabu yao, hawatasamehewa wote wanaojijua watambue Chadema bye bye,” amesema.
Miongoni mwa waliosimamishwa ni aliyekuwa Katibu wa Jimbo la Bumbuli, Abubakari Mashambo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Morogoro, Barnabas Okola, Amuli Shindo, Joseph Mwakidasi na Mathias Cosmas waliokuwa wenyeviti wa Chadema wilaya za Mkinga, Kilindi na Muheza, mkoani Tanga.
Selasini alimwa barua
Katika hatua nyingine, kada mpya wa chama hicho Joseph Selasini amepewa barua na tawi lake la Maharo wilayani Rombo, akitakiwa kujieleza kuhusu tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya chama hicho.
Katika barua hiyo, ambayo Mwananchi imeiona iliyoandikwa na Katibu wa Chadema wa Kata ya Makiidi imetuhumu Selasin kwa kutoa matamko na shutuma dhidi ya Heche bila kufuata utaratibu wa chama wa kuwasilisha malalamiko kwa utaratibu wa Katiba na kanuni.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 6.3 ya Katiba ya Chadema toleo 2019 unatakiwa kujieleza kwa maandishi ndani ya siku 14 sababu zinazopaswa kuzuia kuchukuliwa hatua dhidi yako kutokana na tuhuma hizo.
“Kuanzia tarehe ya kupokea barua hii hauruhusiwi kushiriki, kuongoza kutekeleza shughuli zozote za chama hadi utakaokamilisha utaratibu wa kujieleza na shauri lako litakaposikilizwa,” imeeleza barua hiyo.
Kauli ya Selasini
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Julai 15, 2026, Selasini amesema yeye hakumtuhumu Heche isipokuwa alisema yapo maneno yanayozungumzwa mtandaoni, hivyo ili kuondokana na hayo Chadema kanuni zake.
“Matokeo ya kanuni hizo yatafuta hayo maneno ndicho nilichosema, hakuna mahali niliposema makamu mwenyekiti mwizi au amechukua fedha hakuna mahali popote nimesema.
“Nilichosema kamati ndogo inaweza kuundwa kulingana na Katiba ya chama ili kuchunguza hayo maneno kisha kuja na kauli ya kumsafisha makamu mwenyekiti, sasa kauli kumsafisha mtu ni kumtuhumu kweli,” amesema Selasini.
Selasini ambaye ni mbunge wa zamani wa Rombo amesema hana wasiwasi wamtumie hiyo barua ataiona.
Alichokisema kabla kuandikiwa barua
Jana Julai 14, 2026 Selasini alisema pamoja na kilichoelezwa na Mnyika, lakini wanasiasa hawapaswi kuwa kama mbuni ambaye akisikia gari anaficha kichwa kwenye mchanga akifikiri haonekani ila ukweli haufichiki kwa namna hiyo.
“Kwa sababu Chadema ni chama cha demokrasia, basi hilo jambo litawekwa wazi, chama kina vyombo ili kuwaweka pamoja wanachama na uaminifu ni vizuri vikafanya kazi yake, kazi ikiwa nzuri viongozi wanasafishika,” alisema.
Alisema kiongozi ukishatuhumiwa, hata lugha itumike nzuri kiasi gani, kitu kitakachomfanya kusimama imara kuendelea kuaminika ni vyombo kufanya kazi ya uwazi utakaomwezesha kuwa huru.
“Matumaini yangu baada ya hotuba ya Mnyika, hatua nyingine itafuata ili kuhakikisha dukuduku lililopo mtandaoni linawekwa vizuri. Kosa kubwa lililofanyika NCCR- Mageuzi ni kumtimua kila aliyekuwa anahoji,” alisema Selasini.
Ni mbinu kulinda nidhamu
Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Siasa, Profesa Baraka Mfinanga, amesema hatua ya Chadema kusisitiza nidhamu ya ndani inaonesha chama kinataka kulinda umoja na kuzuia migogoro ya ndani kuhamia kwenye mjadala wa umma, unaoweza kukidhoofisha kisiasa.
Amesema migogoro inapopelekwa kwenye vyombo vya habari kabla ya kujadiliwa ndani ya vikao halali, hujenga taswira ya mgawanyiko na kuibua maswali kuhusu uwezo wa chama kusimamia masuala yake ya ndani.
“Hatua za kuwataka viongozi au wanachama kujieleza si adhabu yenyewe, ni sehemu ya utaratibu wa kutoa haki na kusikiliza pande zote kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika,” amesema.
Hata hivyo, amesema vyama vya siasa vinapaswa kuwa makini kuhakikisha utekelezaji wa nidhamu hauonekani kama njia ya kuzima maoni tofauti, kwa kuwa demokrasia ya ndani huhitaji nafasi ya wanachama kueleza wasiwasi wao.
Profesa Mfinanga, amesema namna Chadema itakavyoshughulikia suala hilo, itakuwa kipimo muhimu kwa umma kuona kama chama kinaweza kuunganisha nidhamu, uwajibikaji na uhuru wa wanachama kueleza hoja zao kwa mujibu wa katiba na kanuni zake.