
Umoja wa Ulaya (EU) umesisitiza tena uungaji mkono wake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), ukipinga kampeni mpya ya utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump ya kudhoofisha mahakama hiyo yenye makao yake makuu The Hague nchini Uholanzi.
Msemaji wa Tume ya Ulaya, Anouar El Anouni amesema msimamo wa kambi hiyo kuhusu ICC haujabadilika, akisisitiza EU inafungamana na mapambano dhidi ya kukwepa adhabu.
“Tunasimama kidete katika kuunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai,” El Anouni amesema, akisisitiza nafasi ya mahakama hiyo katika kuwafungulia mashtaka na kuwahukumu wahusika wa baadhi ya uhalifu mbaya zaidi duniani, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Amesema jaribio lolote la kuidhoofisha mahakama hiyo halikubaliki.
“Mashambulizi au vitisho dhidi ya mahakama, maafisa wake waliochaguliwa, wafanyakazi au wale wanaoshirikiana na mahakama hiyo havikubaliki,” amesema El Anouni.
Akipinga hoja ya Washington kwamba ICC inatishia uhuru wa kitaifa, amesema mahakama hiyo “hailengi mataifa yanayojitawala, wala si tishio kwa mamlaka zao.”
Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kutangaza kampeni ya “kuizima kimfumo” ICC, akiishutumu mahakama hiyo kuwa inaingilia shughuli za kijeshi na utekelezaji wa sheria za Marekani na kudai kwamba inatishia mamlaka ya nchi hiyo.
Mahakama ya ICC, iliyoanzishwa chini ya Mkataba wa Roma wa 1998, inachunguza, kuwafungulia mashtaka na kuwahukumu watu binafsi wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na jinai za uchokozi.
Mnamo Novemba 2024, mahakama hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita, Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na kutenda jinai dhidi ya ubinadamu uliofanywa katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Matukio haya pia yanakuja huku zaidi ya wataalamu 100 wa sheria za kimataifa nchini Marekani wakionya kwamba uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran unaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa.