
Kigoma. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwanasiasa maarufu, Dk Willbrod Slaa, wamefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi na wenzake sita.
TLS na wenzake wamefungua kesi hiyo Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Tabora, chini ya hati ya dharura wakipinga kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni kuhusiana na zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Mbali na Katambi, aliyeshtakiwa kwa jina lake, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Pia, wamewaunganisha wadhamini waliosajiliwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wadhamini waliosajiliwa wa chama cha ACT- Wazalendo.
Juni 26, 2026, akiwa bungeni jijini Dodoma wakati vikao vya Bunge vikiendelea, Waziri katambi alipiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa nchini kote kwa kile alichoeleza ni sababu za kiusalama, akamuelekeza IGP kutekeleza agizo hilo.
Zuio hilo, pia, liliwekewa msisitizo na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali, akiwa katika moja ya ziara zake mkoani Singida.
Kwa mujibu wa walalamikaji, agizo hilo limeanza kutekelezwa na IGP na wasaidizi wake, maofisa au wakala wake.
Wanadai kuwa kauli na maelekezo hayo ni ya kibaguzi na yanakiuka Katiba hasa Ibara za 12, 13(1) (2) na (4) na 29(1) na (2) na zinaingilia uhuru wa kikatiba wa kujieleza kutoa maoni na mawasiliano zinazohifadhiwa na Katiba Ibara ya 18 na uhuru wa raia kushiriki katika masuala ya umma kinyume cha Ibara ya 21(1) na (2) ya Katiba.
Wanadai kuwa Katambi wala Waziri wa Mambo ya Ndani hawana mamlaka ya kikatiba kuzuia haki za kikatiba zinazotolewa na Katiba.
Hivyo, wanaiomba Mahakama itamke kuwa kauli alizozitoa Katambi katika wadhifa wake wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kuzuia mikutano inayoandaliwa na vyama vya siasa kikiwemo Chadema na ACT-Wazalendi, zinakiuka Katiba huku wakibainisha ibara mbalimbali.
Pia, wanaiomba Mahakama itamke kuwa si Katambi wala Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ana mamlaka ya kikatiba wala ya kisheria kuzuia haki hizo za kikatiba.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu, Isaya Arufani (kiongozi wa jopo) Ilvin Mugeta na Martha Mpaze.