NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wazazi na walezi kuimarisha malezi ya watoto na kushiriki kikamilifu kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoathiri wanawake na watoto.
Mahundi amesema malezi bora ni msingi wa kujenga jamii yenye maadili na kwamba watoto wanapaswa kukuzwa katika mazingira salama yatakayowawezesha kuwa raia wema wenye mchango kwa Taifa.
Akizungumza katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, amesema jamii inapaswa kushirikiana kukomesha ukatili wa kijinsia na kulinda haki za watoto. “Tupige kelele kukataa ukatili wa kijinsia na tuwalinde watoto wetu ili wakue katika mazingira salama,” amesema.

Aidha, amewahimiza wananchi kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kusimamia miradi ya kiuchumi ili kuongeza kipato cha familia na kuharakisha maendeleo ya jamii. Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa makundi mbalimbali kupitia mikopo, mafunzo na miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo, Mahundi alitembelea vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na Shule ya Msingi Itumbike yenye kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu, na kuzindua jengo la kivuli katika Soko la Kijiji cha Kanyonza. SOMA: Ukatili wa Kijinsia Unaendelea Kuathiri Jamii