Dar es Salaam. Serikali ya Norway imeidhinisha ruzuku ya Krone 30 milioni za Norway (Sh8 bilioni) kwa Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu Tanzania (TaTEDO-SESO) ili kutekeleza mradi wa miaka mitatu utakaolenga kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Mradi huo wa nishati unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa na nafuu za nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa mijini na vijijini ambao bado hawaitumii sambamba na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Makubaliano ya ruzuku hiyo yamesainiwa leo Alhamisi, Julai 16, 2026 kati ya Ubalozi wa Norway nchini Tanzania na TaTEDO-SESO, ikiwa ni sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu unaolenga kuisaidia Tanzania kufikia malengo ya mpito, kuelekea matumizi ya nishati safi, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati.
Kwa mujibu wa TaTEDO-SESO, mradi huo unatarajiwa kufikia takribani kaya 30,000, taasisi 250, biashara ndogo na za kati pamoja na kuzalisha ajira 2,500, huku asilimia 40 ya nafasi hizo zikitarajiwa kunufaisha wanawake.
Kupitia mradi huo, Tanzania inatarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia, kupanua matumizi ya nishati jadidifu kwa kaya, taasisi na shughuli za uzalishaji, pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na maendeleo ya soko la nishati safi.
Programu hiyo itatekelezwa kuanzia Agosti 2026 hadi Julai 2029, huku ikiunga mkono utekelezaji wa Mission 300 Energy Compact na Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034, unaolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa na kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes amesema ushirikiano huo unaonesha dhamira ya nchi yake ya kuendelea kuisaidia Tanzania kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za nishati safi na endelevu.
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Dar es Salaam ili kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kuharakisha utumiaji wa nishati safi ya kupikia kusaidia wananchi wasiotumia nishati safi waliopo mijini na vijijini. Picha na Sute Kamwelwe
“Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi inayochochea maendeleo endelevu, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi shirikishi kupitia uwekezaji katika sekta ya nishati,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TaTEDO-SESO, Estomih Sawe amesema ruzuku hiyo ni zaidi ya msaada wa kifedha.
Amesema uwekezaji huo wa kimkakati utasaidia kuharakisha utekelezaji wa malengo ya Taifa katika sekta ya nishati.
Sawe amesema mradi huo utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro na Dodoma, maeneo ambayo matumizi ya mkaa bado ni makubwa.
“Mikoa hii ina matumizi makubwa ya mkaa, hususan Dar es Salaam ambayo hutegemea kwa kiasi kikubwa mkaa kutoka Pwani. Tunataka kupunguza utegemezi huo kwa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Sawe.
Amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa suluhisho muhimu la kupunguza ukataji wa misitu, kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi, kuboresha afya ya wananchi kwa kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, pamoja na kuzalisha ajira za kijani, hususan kwa wanawake na vijana.
“Mradi unalenga pia kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi unaokadiriwa kufikia tani kati ya 60,000 na 90,000 za kaboni,” amesema Sawe.
Mbali na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, mradi huo unatarajiwa kuboresha afya ya jamii kwa kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa, kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu, kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi, kuimarisha ustahimilivu wa jamii na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira hatarishi.