
Mwanza. Ni mara ngapi tunashuhudia watu wakienda haja kubwa sana usiku au kuwa na mabadiliko ya mapigo ya moyo ya mara kwa mara?
Wapo watu wanaopitia hali hizi lakini hawaoni umuhimu wa kwenda kupima kujua kile kinachowasibu.
Hawa ndio wale ambao baada ya muda hujikuta wakiwa na hali tete ya maradhi yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, ambayo pengine kama wangewahi mapema kupima au kuwaona wataalamu hadithi ingekuwa tofauti.
Kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza hususani kisukari na shinikizo la damu yameendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za afya katika jamii nyingi duniani na hapa nchini Tanzania.
Magonjwa haya yamekuwa tishio kubwa kwa sababu mara nyingi huanza bila dalili za wazi, hali inayosababisha watu wengi kuishi nayo kwa muda mrefu bila kujua kuwa tayari wana tatizo linaloweza kuharakisha hata maisha yao.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu wa afya duniani wanasisitiza kuwa suluhisho la kwanza katika kupambana na kisukari na shinikizo la damu si kusubiri dalili zijitokeze, bali ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kujua hali ya mwili mapema na kuchukua hatua.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) takribani watu bilioni 1.4 wenye umri wa miaka 30 hadi 79 duniani wanaishi na shinikizo la damu.
Kati ya watu hao, zaidi ya milioni 600 hawajui kuwa wana tatizo hilo, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya kupata madhara yanayoweza kuzuilika.
WHO inaeleza kuwa shinikizo la damu ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo duniani, kutokana na uhusiano wake na magonjwa ya moyo, kiharusi na matatizo mengine ya mfumo wa damu.
Kwa upande wa kisukari, takwimu za Shirikisho la Kisukari Duniani (IDF) za mwaka 2024, zinaonyesha kuwa watu wazima milioni 589 wenye umri wa miaka 20 hadi 79 duniani, wanaishi na ugonjwa huo. Kati yao, takribani milioni 252 hawajui kuwa wana kisukari.
Hali hiyo inaifanya jamii kuwa katika hatari zaidi kwa sababu watu wengi huendelea kuishi bila matibabu wala mabadiliko ya maisha, yanayoweza kusaidia kudhibiti ugonjwa.
Hali ilivyo nchini
Nchini Tanzania, hali ya magonjwa haya imeendelea kuwa changamoto, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa wananchi kupima afya zao mara kwa mara.
Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Zijue Namba Zako” jijini Mwanza Mei mwaka huu, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alisema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazohitaji hatua za pamoja.
Alisema magonjwa haya mara nyingi huanza kimya kimya na watu wengi hugundulika wakiwa tayari katika hatua za juu za ugonjwa.
Akitoa takwimu za ufuatiliaji wa viashiria vya magonjwa yasiyoambukiza kwa mwaka 2023, Waziri Mchengerwa alisema zaidi ya asilimia 73 ya watu wenye shinikizo la juu la damu, hawajui kuwa wanaishi na tatizo hilo, huku takribani asilimia 3.3 pekee ya watu wenye tatizo hilo wanaoweza kulidhibiti ipasavyo.
Kwa Mchengerwa, takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa kubadili mtazamo wa jamii kutoka kusubiri kuugua na kutafuta tiba, kwenda kwenye mfumo wa kinga na uchunguzi wa mapema.
“Shinikizo la damu linaweza kuwa ndani ya mtu bila yeye kujua, kisukari kinaweza kuanza kimya kimya…magonjwa ya moyo yanaweza kukua taratibu,” alisema.
Kupitia kampeni ya “Zijue Namba Zako”, Serikali inawataka wananchi kufahamu viashiria muhimu vya afya zao ikiwemo shinikizo la damu, kiwango cha sukari mwilini, uzito, uwiano wa uzito na kimo pamoja na mzunguko wa kiuno.
Kwanini ni muhimu kupima mara kwa mara?
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kupima mara kwa mara, ni hatua muhimu inayoweza kusaidia kugundua matatizo mapema na kuzuia madhara makubwa.
Dk Osmund Dyegura, Nganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, anasema kila mtu anapaswa kuwa na utaratibu wa kupima kisukari na shinikizo la damu mara kwa mara.
Anasema mtu anayepima mara kwa mara huwa katika nafasi nzuri ya kubaini changamoto, akiwa bado katika hatua za awali na kupata matibabu au ushauri kabla hali haijawa mbaya.
“Wakati mwingine mtu unakuwa na changamoto hizo ila haujijui hadi pale unapoanza kuugua, ambapo ukienda kupima unakuta hali imeshakuwa mbaya wakati kumbe kama ungegundulika mapema, ungepata matibabu mapema na kuzuia hali isiwe mbaya zaidi,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Dyegura, kusubiri hadi dalili zitokee ni hatari kwa sababu baadhi ya madhara yanayotokana na kisukari na presha, yanaweza kuwa makubwa na gharama zake kuwa juu.
Anaeleza kuwa kugundua mapema humwezesha mgonjwa kupata matibabu kwa urahisi zaidi, kutumia gharama ndogo na kuendelea na maisha bila kupata madhara makubwa.
Hili hapa suluhisho
Mbali na maelekezo ya wataalamu, kazi mbalimbali za kitafiti, zimeonyesha kuwa uchunguzi wa mapema pamoja na udhibiti mzuri wa kisukari na shinikizo la damu, vinaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara yanayotokana na magonjwa haya.
Moja ya kazi hizo ni utafiti kuhusu udhibiti wa shinikizo la damu uitwao ‘Systolic Blood Pressure Intervention Trial (SPRINT), uliofanywa nchini Marekani na kuchapishwa mwaka 2015.
Utafiti huo ulihusisha washiriki 9,361 wenye umri wa miaka 50 na zaidi ambao walikuwa katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
Watafiti walilinganisha makundi mawili ya wagonjwa; kundi lililolenga kufikia kiwango cha chini zaidi cha shinikizo la damu na kundi lililofuata kiwango cha kawaida cha udhibiti wa presha.
Matokeo ya utafiti huo yalibaini kuwa kudhibiti shinikizo la damu kwa ukaribu zaidi kulipunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupata matatizo makubwa ya moyo na mishipa ya damu, ikiwemo vifo vinavyotokana na magonjwa hayo.
Utafiti huo ulionyesha kuwa kugundua presha mapema na kuanza udhibiti wa kitaalamu, kunaweza kuwa hatua muhimu ya kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Kwa upande wa kisukari, United Kingdom Prospective Diabetes Study (UKPDS), ni miongoni mwa tafiti kubwa zilizowahi kufanyika kuhusu ugonjwa huo.
Utafiti huu ulifanyika nchini Uingereza na kuchapishwa mwaka 1998 ukihusisha wagonjwa zaidi ya 5,000 waliokuwa wamegundulika kuwa na kisukari aina ya pili.
Watafiti walifuatilia wagonjwa hao kwa miaka kadhaa ili kuona athari za udhibiti wa sukari mwilini na namna ulivyoweza kupunguza madhara ya muda mrefu ya ugonjwa.
Matokeo yalibaini kuwa udhibiti bora wa kiwango cha sukari, ulisaidia kupunguza hatari ya kupata matatizo yanayotokana na kisukari, hususani yale yanayoathiri mishipa ya damu.
Utafiti huo ulitoa ujumbe muhimu kwamba kugundua kisukari mapema na kuanza hatua za kudhibiti ugonjwa, kunaweza kusaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza baadaye.
Faida za kugundua mapema ugonjwa
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, faida ya kwanza ya kupima mara kwa mara, ni kumpa mtu nafasi ya kujua hali yake kabla ya kupata madhara makubwa.
Mtu anayegundulika mapema kuwa ana shinikizo la damu, anaweza kuanza hatua za kudhibiti kama kubadili mtindo wa maisha, kupunguza matumizi ya chumvi, kufanya mazoezi na kutumia dawa anazoelekezwa na mtaalamu wa afya.
Kwa upande wa kisukari, mtu anayegundulika mapema anaweza kuanza kudhibiti kiwango cha sukari mwilini kupitia lishe bora, mazoezi na matibabu kulingana na ushauri wa wataalamu.
Dk Dyegura anasema ugonjwa unapogundulika mapema huwa rahisi zaidi kudhibiti, ikilinganishwa na pale ambapo mtu anafika hospitali akiwa tayari amepata madhara makubwa.
Anasema kuchelewa kugundua magonjwa haya, huongeza mzigo kwa mgonjwa, familia na mfumo wa afya kwa ujumla.
“Mgonjwa akifika mapema tunakuwa na nafasi kubwa ya kumsaidia. Lakini anapofika akiwa tayari amepata madhara makubwa, matibabu yanaweza kuwa magumu zaidi na gharama kuwa kubwa,” anasema.
Aidha, kwa mujibu wa WHO, kudhibiti shinikizo la damu mapema hupunguza hatari ya kupata kiharusi na magonjwa ya moyo.
WHO inasisitiza kuwa kupima presha mara kwa mara ni hatua rahisi lakini yenye uwezo mkubwa wa kugundua tatizo mapema na kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kwa upande wa kisukari, wataalamu wa IDF wanaeleza kuwa kugundua ugonjwa mapema humsaidia mtu kuanza hatua za kudhibiti na kupunguza uwezekano wa kupata madhara kama upofu, matatizo ya figo, uharibifu wa mishipa ya fahamu na magonjwa ya moyo.
Kwa nini familia, nchi na dunia kwa jumla ziingie kwenye gharama kubwa ya kuhudumia wagonjwa wa maradhi ambayo, kimsingi yanaweza kuepukika ikiwa tu watu watajenga utamaduni wa kupima afya na kubadili mitindo ya maisha? Ni wakati sasa wa kuamka na kuchukua hatua dhidi ya wauaji hawa wa kimyakimya.