ALIYEKUWA mshambuliaji wa KMC FC, Daruweshi Saliboko ameibua vita mpya sokoni baada ya Dodoma Jiji kuingilia kati dili hilo na kutaka kupindua, licha ya awali maafande wa JKT Tanzania kuanza mazungumzo na nyota huyo ili kuipata saini yake.
Licha ya KMC kushuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Ligi ya Championship kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kushika nafasi yaa 16 na pointi tisa, ila Saliboko ni miongoni mwa washambuliaji waliofanya vizuri akiwa na kikosi hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson amesema taratibu zote za kukamilisha baadhi ya wachezaji wapya zinaendelea, hivyo, muda wowote kuanzia sasa wataanza kuwatangaza wote waliofikia makubaliano nao rasmi.
“Taratibu zote zikikamilika kila kitu tutakiweka wazi, wapo wachezaji tunaendelea na mazungumzo nao na tutakapokamilisha mashabiki zetu wataona, huu ni muda sahihi wa usajili na ni lazima tuufanye kwa umakini pia mkubwa,” amesema Fortunatus.
Mwanaspoti linatambua, Saliboko aliyeifungia KMC FC mabao manne ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, alikuwa mbioni kujiunga na JKT Tanzania, ingawa, baada ya Dodoma Jiji kuonyesha nia ya kumuhitaji pia kwa sasa chaguo limebakia kwake.