RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Misri zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji kupitia maendeleo ya miundombinu, hatua inayolenga kurahisisha biashara kati ya nchi hizo mbili na kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa kwenda katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa Makubaliano wa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya uchukuzi, Dk. Samia amesema makubaliano hayo yataimarisha ufanisi wa usafirishaji wa mizigo, kuongeza biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Misri.
“Tumekubaliana kuunganisha bandari zetu. Bandari ya Dar es Salaam watatusaidia katika maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Aidha, kupitia mazungumzo haya, kutakuwa na ujenzi wa reli itakayounganisha Bandari ya Bagamoyo na Bandari Kavu ya Kwala, ambako pia kutakuwa na maeneo ya kuhifadhi mizigo yao,” alisema Dk. Samia.
Rais Samia amesema ushirikiano huo unahusisha kuimarisha shughuli za Bandari ya Dar es Salaam, maendeleo ya Bandari ya Bagamoyo na ujenzi wa reli ya kuiunganisha Bandari ya Bagamoyo na Bandari Kavu ya Kwala, hatua inayotarajiwa kuboresha mnyororo wa usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini hadi maeneo ya ndani ya nchi na masoko ya kikanda.
Amesema utekelezaji wa makubaliano hayo pia utarahisisha usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Misri, kuongeza ushindani wa bidhaa katika masoko ya kimataifa, kufungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili na Bara la Afrika kwa ujumla.
Naye Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Abdel Fattah El-Sisi amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Misri utafungua fursa mpya za biashara na uwekezaji, huku ukiendeleza historia ya uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi uliodumu kwa miaka mingi kati ya mataifa hayo mawili. “Serikali yetu iko tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta za uchumi, nishati na biashara. Tutaendelea kuimarisha ushirikiano huu kwa maslahi ya watu wetu,” alisema Rais Abdel Fattah El-Sisi.
SOMA: Naibu Waziri Nishati ashiriki mkutano Misri
