UKIWAULIZA mashabiki wa Yanga kuna mchezaji gani wanamsubiri basi jibu lao kubwa litakuwa ni hili tu nani atakuwa kiungo wao namba sita pale kati na hesabu hizo ndio zinawapasua vichwa pia mabosi wao wakipiga hesabu za kurudi Azam FC kumfuata kiungo mmoja wa kazi.

Mashabiki wa Yanga wana kiu kubwa ya kuona katika harakati za usajili unaofanywa kwa msimu ujao basi analetwa kiungo mkabaji ambaye atakuja kuirudishia ubora timu hiyo kwenye mashindano yanayokuja.

Tangu kuondoka kwa Khalid Aucho Yanga imeshindwa kupata kiungo wa shoka aliyeziba nafasi ya raia huyo wa Uganda  baada ya usajili wa Moussa Bala Conte kushindwa kukidhi kiu ya eneo hilo na kuondoilewa akitolewa kwa mkopo Raja Athletic ya Morocco.

Baada ya kufeli wa Bala Conte Yanga ikamleta Mahammed Damaro akitokea Singida Black Stars lakini naye akashindwa kuwashawishi mabosi wa klabu hiyo kocha na hata mashabiki, kivuli cha Aucho kikiendelea kuitesa klabu hiyo.

Yanga sasa uhakika itamuacha kwa kumrudisha klabuni kwake Damaro ambaye alitua hapo na kucheza nusu msimu tu katika mzunguko wa pili msimu uliopita.

Mabosi wa Yanga bado wanapambana kutafuta watu sahihi wa eneo hilo ambapo wakati msako ukiendelea kwa mastaa wa nje, sasa kuna hesabu za kutafuta nafasi ya kumpata Adolf Mtasingwa aliyepo pale Azam FC.

Yanga imewahi kufanya mazungumzo na Mtasingwa msimu uliopita wakati huo akibakisha mkataba wa miezi sita na matajiri hao wa Chamazi lakini baadaye akaongeza mkataba wa mwaka mmoja zaidi kusalia Azam FC.

Yanga wanapiga hesabu kwamba kama wakimpata kiungo huyo watakuwa wamepata chaguo sahihi kwa wachezaji wa ndani wanaocheza eneo hilo huku wakitafuta kiungo mkabaji wa kigeni ambaye atakuwa na uwezo wa kucheza kama beki wa kati.

“Yule Mtasingwa ni mchezaji muafaka sana kwetu lakini hatujakata tamaa tunafikiria ni namna gani tunaweza kupata huduma yake, bahati mbaya sana alifanya papara akaongeza mkataba mwingine wa mwaka mmoja ndio huu unatupasua kichwa,”amesema bosi huyo wa juu wa Yanga.

“Kama tukifanikiwa kumpata itakuwa sawasawa kwetu lakini hatuna uhakika kama Azam itakubali kumuachia, tutajaribu, kwa wachezaji wa kigeni bado tunatafuta pia mtu mwingine kama tutapata mtu sahihi.

Azam chini ya kocha Florent  Ibenge Mutasingwa amekuwa akisotea benchi zaidi tangu arudi kutoka majeruhi ambapo msimu uliomalizika alifanikiwa kucheza mechi sita pekee  akitumia dakika 297 ambapo katika mechi hizo ni mechi tatu za mwisho ndizo alizofanikiwa kumaliza dakika 90 kila moja.

Kama wakifanikiwa utakuwa usajili mwingine wa mchezaji mkubwa kutoka Azam baada ya jana Simba kumtangaza Nathan Chilambo akitokea hapohapo Azam, ukiwa ni usajili ambao Mwanaspoti iliuripoti tangu Machi 2026 kuwa Simba imeshamalizana naye. Endelea kutuamini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *