UNAWEZA kusema sasa ni vuta nikuvute ya usajili wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar zikifanya mageuzi ya kujiandaa na msimu wa 2026-2027.

Katika hali hiyo, timu ya Chipukizi yenye makazi yake kisiwani Pemba, imeachana na wachezaji 12 huku ikiingiza wapya 10.

Wachezaji walioondoka ni Mashir Khamis Sabur, Ayoub Moh’d Abdallah, Job Song, Bille Mwakysa, Sadat Abdallah, Omar Kanyoro, Ali Moh’d Ali, Morata, Abdulraut Haji Makame, Mahir Khamis Sabur, Said Suleiman Matar na Shaban Ali Geda.

Akizungumza na Mwanaspoti, ofisa habari wa timu hiyo, Heri Kidema amesema kuachwa kwa wachezaji hao ni katika hatua za kuisuka timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

“Tunafanya mabadiliko hayo kwa sababu tunahitaji kushindana zaidi msimu ujao na sio kupambana kutoshuka daraja kama ilivyo miaka iliyopita,” amesema.

Ofisa huyo, amesema kwa sasa hawatotaja majina ya wachezaji wapya waliosajiliwa hadi timu itakapowatangaza rasmi.

Alifafanua, timu hiyo imefanya usajili ambao wanaamini watakwenda kurudisha heshima na hadhi ya timu hiyo msimu ujao.

Amesema usajili huo umeangalia zaidi uhitaji wa timu na hawajafanya kwa kukurupuka bali wametathmini wanachokitaka ndicho walichokitafuta.

Hivyo, amewasihi mashabiki wa timu hiyo kusubiria mazuri kutoka kwao na kuwa tayari kuwapokea kwa msimu ujao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *