Dar es Salaam. Mashahidi wawili katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu wameieleza Mahakama Kuu Masjala Kuu ya Dodoma jinsi walivyozuiwa na askari wa Gereza la Ukonga kumkabidhi Lissu nyaraka, ikiwamo iliyotoka Jumuiya ya Madola.

Mashahidi hao ambao pia ni walalamikaji katika kesi hiyo, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, wameelezea mazingira wanayokabiliana nayo wanapokwenda gerezani hapo kushauriana na mteja wao masuala mbalimbali ya kisheria jinsi yasivyo ya faragha.

Mawakili hao wametoa ushahidi huo walipohojiwa na Lissu kuhusu madai yao kwenye hati ya madai na viapo vyao vinavyounga mkono hati hiyo.

Mbali na Nkungu na Kisabo, mdai mwingine katika kesi hiyo ya kikatiba namba 7300/2026 iliyosikilizwa leo Julai 21, 2026 ni wakili Kulwa Maduhu.

Wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), Mkuu wa Gereza la Ukonga, Lissu aliyeunganishwa katika shauri hilo kama mdaawa muhimu pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kilichoomba na kuunganishwa kama mdaawa mwenye masilahi.

Walalamikaji hao wanaojitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu wanadai kuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga ameshindwa kutekeleza Kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza, ambayo inatoa haki kwa mawakili kufanya mashauriano ya siri na wateja wao bila kuingiliwa.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Amir Mruma (kiongozi wa jopo), Dk Angelo Rumisha na Dk Everist Longopa, linaloketi Dar es Salaam.

Mahakama ilipanga kesi hiyo pamoja na pingamizi lililoibuliwa na Serikali lisikilizwe kwa njia ya maandishi, lakini Lissu aliomba na karuhusiwa kuwafanyia mahojiano ya maswali ya dodoso wadai katika kesi hiyo pamoja na mdaiwa wa tatu, Mkuu wa Gereza la Ukonga.

Lissu aliwahoji wadai hao waliosimama kama mashahidi, akianza na wakili Maduhu akiwa wa kwanza miongoni mwa wanne ambao ameomba kuwahoji. Leo Julai 21 ameendelea na wawili ambao ni Nkungu na Kisabo.

Kwa nyakati tofauti akiwahoji mashahidi hao, Lissu ameanza na maswali akiwaongoza kuithibitishia mahakama kwamba kweli wao ni mawakili wake katika kesi zinazomkabili.

Kesi hizo ni ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni inayosikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na ya uhaini inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam.

Kisha aliwahoji maswali mengine yaliyowaongoza kuelezea mazingira yalivyo wanapofika kushauriana naye na nyaraka walizompelekea zikazuiwa na maofisa wa Magereza.

Awali, kabla ya kuanza kumuuliza maswali shahidi, Jaji Mruma alimuuliza Lissu iwapo eneo aliloketi lilikuwa linamfaa naye akajibu linafaa.

Lissu aliketi nje ya kizimba pembeni mwa mawakili wa pande zote ambako aliwekewa meza. Kesi hiyo si ya jinai hivyo hakuwa kizimbani.

Baada ya hilo, Lissu amemtaka shahidi kuieleza mahakama kama yeye ni miongoni mwa mawakili wake katika mashauri yanayonikabili Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Nkungu amejibu kuwa yeye ni mmoja wa mawakili hao na amemtembelea katika Gereza la Ukonga mara 13.

Mahojiano yaliendelea na sehemu yake ni kama ifuatavyo:

Lissu: Eleza mahakama kama una nyaraka zote zinazohusiana na shauri hili.

Nkungu: Ninazo nyaraka zote.

Lissu:  Chukua nakala ya hati yako ya madai na kiapo, umedai kuwa wewe ni mmoja wa mawakili katika kesi zinazonikabili Mahakama Kuu na Mahakama ya Kisutu.

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Kwenye kiapo kinzani cha mdaiwa wa tatu wamekana kuwa wewe na wenzako si mawakili wangu?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Angalia kumbukumbu za Mahakama ya Kisutu za Aprili 24, 2025 mbele ya Hakimu Franco. Ulikuwa mmoja wa mawakili walioniwakilisha siku hiyo?

Nkungu: Kwa kumbukumbu za mahakama, ni kweli.

Lissu: Paul Kisabo alikuwepo siku hiyo?

Nkungu: Alikuwepo.

Lissu: Waeleze majaji kama umenitembelea Gereza la Ukonga mara 13.

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Ulizuiwa hata mara moja kuja kuniona?

Nkungu: Hapana.

Lissu: Wewe upo kwenye orodha ya mawakili walioruhusiwa kunitembelea gerezani?

Nkungu: Nipo, namba saba.

Lissu: Kati ya Aprili 18 na Juni 16 tulikuwa tunaonana ana kwa ana au kwa simu?

Nkungu: Tulikuwa tumetenganishwa na ukuta wa kioo na tulizungumza kwa simu ya mezani.

Lissu: Maofisa wa magereza walikuwepo wakati wa mazungumzo?

Nkungu: Walikuwepo.

Lissu: Mliweza kubadilishana nyaraka?

Nkungu: Hapana.

Lissu: Baada ya Juni 16 mashauriano yalihamishiwa ofisi ya usajili wa wafungwa?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Chumba hicho kilikuwa na askari na kamera za CCTV?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Baada ya Novemba 14, 2025 mashauriano yalihamishiwa ofisi ya Naibu Mkuu wa Gereza?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Mazungumzo yetu yalifanyika mbele ya Mkuu wa Gereza na maofisa wengine?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Miongoni mwa nyaraka mlizoniletea kulikuwa na ripoti ya Tume ya Jaji Chande?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Ripoti hiyo ilichukuliwa na maofisa wa magereza?

Nkungu: Ni kweli.

Lissu: Kama sijapewa ripoti hiyo, naweza kuandaa utetezi wangu?

Nkungu: Huwezi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi Stanley Kalokola anayewatetea wadaiwa wa kwanza mpaka wa watatu alifuata kumhoji na sehemu ya mahojiano yao ni kama ifuatavyo:

Kalokola: Umejitambulisha kuwa wewe ni wakili?

Nkungu: Ni sahihi.

Kalokola: Shauri hili ni la kikatiba, si la uhaini?

Nkungu: Ni sahihi.

Kalokola: Kanuni ya 61 ya Mandela Rules imetaja ukubwa wa chumba cha mawasiliano ya wakili na mteja?

Nkungu: Haijataja.

Kalokola: Sheria ya Magereza inaruhusu ukaguzi wa wanaoingia gerezani?

Nkungu: Inaruhusu ukaguzi.

Kalokola: Kuna katazo kwa maofisa wa magereza kukagua nyaraka?

Nkungu: Sheria za mawakili haziruhusu kukagua mawasiliano ya wakili na mteja.

Kalokola: Sheria za Magereza hazijafafanua ofisi ndogo ni ipi na kubwa ni ipi?

Nkungu: Upo sahihi.

Baadaye Lissu amemhoji shahidi wa tatu, Kisabo na sehemu ya mahojiano hayo ni kama ifuatavyo:

Lissu: Shahidi, Bwana Jela amesema hakuna ushahidi kuwa wewe ni wakili wangu. Ni kweli au si kweli?

Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Pamoja na madai hayo, umekuwa ukija Gereza la Ukonga

kunitembelea mara nyingi?

Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Umekuwa ukiniletea fedha za chakula na mahitaji mengine?

Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Mara ya mwisho uliniletea fedha lini?

Kisabo: Julai 14.

Lissu: Fedha hizo huzikabidhi kwangu au kwa maofisa wa magereza?

Kisabo: Nawakabidhi maofisa wa magereza.

Lissu: Kwenye kumbukumbu za Mahakama ya Kisutu jina lako lilikuwepo kama wakili wangu?

Kisabo: Lilikuwepo.

Lissu: Ulipaswa kumpelekea Mkuu wa Gereza uthibitisho kwamba wewe ni wakili wangu?

Kisabo: Hapana.

Lissu: Ukifanya hivyo utakuwa unakiuka maadili ya wakili na mteja?

Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Ulileta nyaraka kutoka Jumuiya ya Madola zinazohusu kesi yangu?

Kisabo: Ni kweli.

Lissu: Kilitokea nini ulipojaribu kunikabidhi nyaraka hizo?

Kisabo: Maofisa wa magereza walizichukua, wakazisoma na kunizuia nisizikabidhi.

Lissu: Walikupa sababu?

Kisabo: Hapana.

Mbali na mahojiano hayo, Lissu ameeleza namna anapopelekwa mahakamani katika kesi ya uhaini inayomkabili ambavyo mawakili wake hawawezi kuonana naye akiwa mahabusu na ilivyo ngumu kumpa nyaraka mahakamani hapo.

Kesi hiyo itaendelea kesho Jumatano ambapo Mkuu wa Gereza la Ukonga, ambaye ni mmoja wa wadaiwa katika kesi hiyo anatarajiwa kutoa ushahidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *