Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza ongezeko la nauli za usafiri wa umma kwa wastani wa asilimia 16 kwa safari za masafa marefu na mafupi.

Mabadiliko hayo ya nauli na bei elekezi yataanza kutumika Agosti mosi, 2026.

Akitangaza mabadiliko hayo leo Jumanne, Julai 21, 2026, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed, amesema katika viwango vipya, nauli ya daladala imeongezeka kutoka Sh500 hadi Sh700.

Kwa mabasi ya umeme, nauli pia itakuwa Sh700, huku wanafunzi na wazee wakilipia nusu ya nauli hiyo.

“Serikali imefanya mapitio ya viwango vya nauli za vyombo vya usafiri wa umma barabarani, ikiwemo daladala na magari ya shamba, baada ya kufanya tathmini ya hali halisi ya gharama za uendeshaji wa huduma hizo,” amesema.

Amesema katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za uendeshaji wa vyombo vya moto kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia.

Hali hiyo, kwa mujibu wa waziri, imeathiri uwezo wa baadhi ya watoa huduma kuendesha shughuli zao kwa ufanisi, jambo lililopelekea Serikali kupokea maombi kutoka kwa jumuiya za usafirishaji za Unguja na Pemba kuhusu marekebisho ya viwango vya nauli.

“Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, mapendekezo hayo yalifanyiwa uchambuzi wa kina kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili, yaani wananchi wanaotumia huduma za usafiri na watoa huduma wanaowezesha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu,” amesema.

Akitaja marekebisho hayo ya nauli, Dk Khalid amesema kwa safari za umbali mfupi wa kilomita moja hadi 12, nauli imeongezeka kutoka Sh500 hadi Sh700.

Aidha, kwa safari za umbali mrefu wa kilomita 19 hadi 21, nauli imebadilika kutoka Sh800 hadi kufikia Sh1,000.

Kwa upande wa magari ya shamba, kwa safari za umbali mfupi wa kilomita moja hadi 14, nauli imeongezeka kutoka Sh600 hadi Sh700.

Aidha, kwa umbali wa kilomita 60 hadi 70, nauli imebadilika kutoka Sh2,500 hadi Sh3,000.

Kwa upande wa mabasi ya umeme, amesema safari kutoka kituo cha Malindi hadi Buyu itagharimu Sh700, huku safari kutoka Malindi hadi Uwanja wa Ndege nayo ikiwa Sh700. Wanafunzi na wazee wataendelea kulipa nusu ya nauli hiyo.

Aidha, amezitaka jumuiya za usafirishaji Unguja na Pemba kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani kuhakikisha mchanganuo wa nauli kwa kila njia unaandaliwa, unathibitishwa na kuwekwa wazi katika kila chombo cha usafiri wa umma ili kuondoa mkanganyiko na migogoro isiyo ya lazima.

Wakati wadau wa usafirishaji wakipongeza hatua hiyo, baadhi ya wananchi wamesema ongezeko hilo linaweza kuwa mzigo kwao kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Khatib Juma Haji, dereva na mmiliki wa daladala, amesema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakifanya biashara kwa hasara kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za mafuta, huku nauli ikiwa haijabadilika.

Shuweina Abubakar, mkazi wa Jang’ombe, amesema kupanda kwa nauli kutazidi kuwaumiza wananchi wa hali ya chini kutokana na uwezo wao mdogo wa kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *