Magazeti ya Jumatano, tarehe 22 Julai, yaliripoti kuhusu mada mbalimbali, ikiwemo kutoridhishwa kwa walimu kuhusu fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya nyongeza ya mishahara yao.

Kenyan newspapers.
Front pages of Daily Nation and The Star newspapers. Photos: Screengrabs from Daily Nation, The Star.
Source: UGC

1. Daily Nation

Walimu kote nchini wamekataa awamu ya pili ya nyongeza ya mishahara chini ya Mkataba wa Pamoja wa Majadiliano ya Mishahara (CBA) wa 2025–2029, wakisema kiwango hicho ni kidogo mno na hakilingani na kupanda kwa gharama ya maisha.

Malalamiko hayo yalizuka baada ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kutoa mwongozo wa kutekeleza awamu ya pili ya makubaliano hayo kuanzia Julai 1, 2026.

Walimu wengi walibaini kuwa nyongeza halisi ya mishahara yao ilikuwa kati ya KSh 693 na KSh 2,055 kulingana na daraja la kazi na kiwango cha mshahara.

Ingawa serikali ilitenga KSh 8.4 bilioni kutekeleza awamu hiyo, walimu wanasema kiasi kinachoingia kwenye akaunti zao baada ya makato ya kisheria hakionyeshi tofauti kubwa na mishahara yao ya awali.

“Mwalimu wa daraja la C3 alipangiwa nyongeza ya KSh 2,055, lakini kiasi hicho ni kabla ya makato ya PAYE, SHA, Ushuru wa Nyumba na NSSF. Kinachobaki ni kidogo mno na hakiwezi hata kulipia mkopo wa SACCO,” alisema mwalimu mmoja kutoka Nairobi.

Pia soma

Magazetini: Ndani ya muundo mpya wa mishahara ya walimu baada ya TSC kutekeleza CBA mpya

Mkataba huo wa miaka minne una thamani ya KSh 33.75 bilioni na unahusisha nyongeza za mishahara pamoja na masuala ya ustawi wa walimu.

Hata hivyo, walimu wengi sasa wanahisi matarajio yaliyowekwa na vyama vyao vya wafanyakazi hayalingani na hali halisi.

Katibu wa tawi la KUPPET Vihiga, Sabala Inyeni, alisema nyongeza hiyo haijazingatia mfumuko wa bei wala ongezeko la gharama za usafiri.

“Marupurupu ya usafiri hayajarekebishwa kwa zaidi ya miaka 15 ilhali bei ya mafuta imeendelea kupanda. Ongezeko hili haliakisi uhalisia wa gharama ya maisha,” alisema.

Walimu wanaofanya kazi katika maeneo ya ukame na yenye mazingira magumu pia walieleza kutoridhishwa kwao baada ya marupurupu ya mazingira magumu kutoongezwa.

Katibu wa chama kinachowawakilisha walimu katika maeneo hayo, Ndung’u Wangenye, alisema baadhi ya walimu waliongezewa chini ya KSh 500 licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu.

“Walimu katika maeneo kame wanahisi kusalitiwa. Marupurupu ya mazingira magumu ndiyo yanawapa motisha ya kuendelea kufanya kazi huko, lakini hayajaguswa kabisa,” alisema.

Naibu Katibu Mkuu wa KUPPET, Moses Nthurima, alisema walimu wengi hawajaridhishwa na matokeo ya mazungumzo ya Mkataba wa Pamoja wa Majadiliano ya Mishahara (CBA).

Pia soma

Betty Maina adokeza kuhusu kurudisha boti za serikali baada ya UDA ‘kuoshwa’ Ol Kalou

2. Taifa Leo

Gazeti hili liliripoti kuwa Rais William Ruto aliikosoa Mahakama kwa kile alichokitaja kuwa kutoa dhamana nafuu kwa washukiwa wa uhalifu wanaotuhumiwa kuvuruga mikutano ya kisiasa, akisema hatua hiyo imechangia kuongezeka kwa uhuni nchini.

Akizungumza Ikulu, Nairobi, Jumanne, rais alisema washukiwa wanaokamatwa kwa makosa ya jinai hupelekwa mahakamani, hupewa dhamana ndogo na kurejea mitaani kuendelea na vitendo vyao.

“Vijana wanaokamatwa kwa uhalifu hupelekwa mahakamani, wanapewa dhamana ya Sh200 na kuachiliwa kwa sababu ni watoto wetu. Kisha wanarudi kwenye mikutano ya kisiasa na kuendelea na vitendo vya uhuni,” alisema Ruto.

Alisema Kenya inapaswa kufanya mjadala wa kina kuhusu ongezeko la uhuni huku joto la kisiasa likizidi kupanda kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini waliohusika na vurugu hizo.

3. The Star

Kaunti za Bungoma na Trans Nzoia zinajiandaa kwa wiki yenye shughuli nyingi za kisiasa huku maandalizi yakikamilishwa kwa ziara ya Seneta Edwin Sifuna mnamo Julai 25 na 26.

Pia soma

Magazeti ya Kenya: IEBC yasema ‘zawadi’ za serikali mara nyingi si rushwa kwa wapiga kura

Tukio hilo limebadilika kutoka ziara ya kawaida hadi kuwa uwanja muhimu wa mapambano ya ushawishi katika eneo la Magharibi mwa Kenya, likiambatana na maandamano ya vijana, nyimbo za kampeni na malori yenye chapa zinazomuunga mkono Sifuna kuwa rais na Mbunge Tim Wanyonyi kuwa gavana.

Wafuasi wa Sifuna wamekumbatia kauli mbiu ya “We are Sifuna” kuashiria uungwaji mkono mkubwa wa eneo hilo, lakini msisimko huo umeandamana na mvutano unaozidi kuongezeka.

Makundi ya vijana pamoja na Mbunge Jack Wamboka wamewaonya wapinzani dhidi ya kuandaa mikutano sambamba au kujaribu kuvuruga mkutano mkuu utakaofanyika Bungoma Posta Grounds.

Wakati huo huo, Mbunge John Waluke aliwaonya wapinzani wa kisiasa dhidi ya kuingilia eneo lake la ushawishi na akamkosoa Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kwa kile alichodai ni kujaribu kutumia umaarufu wa Sifuna kwa manufaa yake.

Kujibu mvutano huo, viongozi wa Linda Mwananchi, akiwemo aliyekuwa Naibu Gavana Charles Ngome, walisisitiza kuwa misingi ya demokrasia inampa kila Mkenya haki ya kufanya mikutano ya amani popote nchini.

Kadiri Magharibi mwa Kenya inavyozidi kuwa kitovu cha mjadala wa kisiasa nchini, macho yote sasa yanaelekezwa kuona iwapo ziara ya Sifuna italeta umoja au itaongeza mgawanyiko uliopo katika eneo hilo.

4. The Standard

Pia soma

Jamaa Amvaa Francis Atwoli kwa kula bata wakati Wakenya wengine wanapitia mateso ya umaskini

Wanafunzi wote watakaofuzu kujiunga na vyuo vikuu vya humu nchini watapata ufadhili kamili wa serikali kwa masomo yao iwapo pendekezo jipya la ufadhili wa elimu ya juu litapitishwa na Bunge.

Rais William Ruto alitangaza hatua hiyo Jumanne akiwa Ikulu, akisema serikali imewasilisha marekebisho ya sheria yatakayohakikisha kila mwanafunzi anayefaulu mtihani wa kitaifa na kupata nafasi katika chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu anafadhiliwa kikamilifu, bila kujali hali ya kifedha ya wazazi wake.

“Kwa sasa tuna pendekezo lililo Bungeni litakalofanya elimu ya juu ipatikane kwa wote. Haitajalisha mtoto anatoka katika familia gani, bali uwezo wake kitaaluma. Mwanafunzi yeyote atakayefaulu na kupata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu atapata ufadhili kamili,” alisema Ruto.

Aliwahimiza wabunge kuharakisha kupitisha marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) ili wanafunzi wanaoanza masomo yao Septemba mwaka huu wanufaike na mfumo huo mpya.

Tangazo hilo linaashiria mabadiliko yanayowezekana kutoka mfumo wa sasa wa ufadhili wa elimu ya juu ulioanzishwa mwaka 2023, ambao umekosolewa na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu.

Rais alisema mfumo wa awali ulishindwa kwa sababu uliyaacha vyuo vikuu vikikumbwa na matatizo ya kifedha baada ya serikali kushindwa kutoa fedha ilizoahidi.

Pia soma

Good Testimony Schools: Kiasi cha karo anacholipa Bahati katika shule anayosomea bintiye Mueni

“Baadaye tulianzisha mfumo wa usawa ambapo wazazi walichangia sehemu ya karo, serikali ikatoa sehemu kupitia ufadhili wa masomo na salio kupitia mikopo. Tuliamini ungeleta usawa, lakini umeonekana kutotosha,” alisema.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *