ETDCO yakamilisha mradi wa umeme kabla ya mudaETDCO yakamilisha mradi wa umeme kabla ya muda

MTWARA: KAMPUNI ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa laini maalum ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 33 kutoka Masasi hadi Newala, Mkoa wa Mtwara, ndani ya miezi saba badala ya miezi 12 iliyokuwa imeainishwa kwenye mkataba.

Hatua hiyo imepongezwa na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana  mkoani Mtwara na kusema utekelezaji huo unaonesha uwezo wa kampuni za ndani kutekeleza miradi ya kimkakati kwa ufanisi na kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Ndejembi amewataka  wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme nchini kufanya kazi kwa weledi, ubora na kuzingatia muda wa mikataba ili kuharakisha utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Amesema serikali inaendelea kuwekeza katika miradi ya umeme ili kuimarisha huduma kwa wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema mradi huo wenye urefu wa takribani kilomita 76 ulikamilika ndani ya miezi saba kutokana na usimamizi mzuri wa kazi, ushirikiano wa wadau na kujituma kwa wataalamu wa kampuni hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameipongeza  ETDCO kwa kuendelea kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati na kwa ufanisi.

Amesema serikali inaendelea na miradi mingine ya kuimarisha upatikanaji wa umeme katika ukanda wa kusini, ikiwemo mradi wa laini ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kutoka Masasi hadi Mahumbika.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi huo wa kilomita 76 utaboresha upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Newala na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.

Ameongeza kuwa TANESCO inatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha kupooza umeme wilayani Newala wenye thamani ya shilingi bilioni 5.27 ili kuongeza uthabiti wa huduma ya umeme.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mbunge wa Newala Vijijini, Dkt. Yahya Nawanda, amesema mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 4.6 utakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo kupitia sekta za viwanda, kilimo na ajira.

Wakazi wa Newala nao wameishukuru Serikali kwa kukamilisha mradi huo, wakisema utaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kufungua fursa zaidi za uzalishaji na uwekezaji katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *