TANGA: WIZARA ya Maji imetangaza mikakati ya kuanzisha mfumo mpya wa upatikanaji wa fedha ujulikanao kama Alternative Financing, ikiwa ni jitihada za makusudi za kuharakisha ukamilishaji wa miradi mikubwa ya maji nchini na kuwaondolea wananchi kero ya ukosefu wa huduma safi na salama kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maji, Juma Aweso, jijini Tanga wakati wa ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Nadir Abdulatif Alwardy, aliyefika mkoani Tanga kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Aweso alieleza kuwa wizara imeamua kubuni njia mbadala za kiubunifu za kujipatia fedha badala ya kutegemea vyanzo vya kawaida vya kibajeti pekee.
“Hatuna sababu ya miradi ya milioni 300 au milioni 400 kuanza kuomba wizara fedha wakati tuna mfumo madhubuti wa kuweza kupata fedha na wananchi wakapata huduma kwa uhakika,”alisema Waziri Aweso.
Aidha, aliongeza kuwa mfumo huo unalenga kwa kiasi kikubwa kushirikisha na Sekta Binafsi katika kugharamia miradi ya maji ili kuondoa kabisa changamoto ya uhaba wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali.
Akizungumzia mafanikio ya Mkoa wa Tanga, Waziri Aweso alieleza kuwa utendaji mzuri uliopatikana katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Hatifungani ni kielelezo na mtindo bora unaopaswa kuigwa na mikoa mingine nchini, ikiwemo Arusha na Mwanza.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Nadir Abdulatif Alwardy, alisema ziara hiyo ni chachu kubwa ya kubadilishana uzoefu na teknolojia ya kisasa katika usimamizi na utoaji wa huduma za maji, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa katika sekta hiyo.
Alisema kuwa Zanzibar itatumia ubunifu na mbinu zilizoshuhudiwa ili kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya maji, kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa haraka na kulinda uendelevu wa miradi.
“Tumekuja kujifunza namna bora ya uendeshaji wa sekta ya maji kwa upande wa Tanzania Bara; hivyo, tutatumia uzoefu huo kuweza kuleta mapinduzi kwa upande wa Zanzibar,”alisema Waziri Alwardy.
Hata hivyo Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Jiji la Tanga Tanga UWASA Dkt Ali Fungo alisema kuwa mradi ya Hatifungani ni ubunifu wa mamlaka hiyo katika kuhakikisha wanatoa huduma bora ya maji kwa wananchi wa jiji la Tanga.
“Kupitia hatifungani tumejifunza nidhamu ya fedha lakini na kumbe watanzania tunaweza kujiletea maendelea wenyewe kupitia fursa ya fedha za hatifungani “alisema Dkt Fungo
