KOCHA wa zamani wa Yanga, Romain Folz, ametaja sababu zilizomfanya amteue raia wa Afrika Kusini, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’, kuwa sehemu ya benchi lake la ufundi katika klabu ya US Monastir ya nchini Tunisia.

Folz hivi karibuni alitangazwa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Tunisia (Ligue Professionnelle 1), baada ya kukaa kwa miezi kadhaa bila klabu huku akitafakari hatua yake inayofuata katika kazi yake ya ukocha.

Kuelekea msimu wa 2026-2027, kocha huyo raia wa Ufaransa ameamua kufanya kazi tena na mtu anayemfahamu vizuri kwa kumteua Skudu aliyewahi kucheza Yanga katika msimu wa 2023-2024.

FOL 01

Skudu ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu kucheza soka la ushindani kufuatia kumalizika kwa kipindi chake cha kucheza katika klabu ya Siwelele msimu uliopita, sasa ameteuliwa kuwa mchambuzi wa kiwango cha uchezaji (performance analyst) katika benchi la ufundi la US Monastir.

Folz aliyeifundisha Yanga msimu wa 2025-2026 akidumu kwa takribani miezi mitatu kuanzia Julai 14, 2025 hadi Oktoba 31, 2025, amesema uhusiano wake na Skudu ulianza walipokuwa pamoja katika klabu ya Marumo Gallants, ambako aligundua mapema uwezo wake wa kuingia kwenye taaluma ya ukocha.

FOL 02

“Nimemfahamu Mahlatse tangu nikiwa Marumo Gallants. Nilikutana na mchezaji bora, lakini zaidi ya yote nikakutana na mtu mwenye utu mkubwa. Ni mtu wa kipekee mwenye uelewa mkubwa wa mchezo,” amesema Folz katika mahojiano maalumu na KickOff.com.

“Niliona uwezo wake wa kuwa kocha mapema na nikamshauri aanze kusomea kozi za ukocha.”

FOL 03

Folz amesema amekuwa akimsaidia Skudu katika safari hiyo kwa miaka kadhaa, jambo lililomsaidia kukuza ujuzi wake na kuongeza maarifa yake ya mbinu za mchezo.

“Nilimsaidia kufuata njia hiyo katika miaka michache iliyopita, na ameendelea kuboresha uwezo wake pamoja na kuongeza uelewa wake wa kiufundi.

“Amemaliza kozi kadhaa ngumu, ikiwemo mafunzo mbalimbali ya kiwango cha juu kuhusu uchambuzi wa mchezo,” amesema Folz.
Kocha huyo wa zamani wa AmaZulu FC, amesema Skudu anastahili nafasi hiyo na anaamini atakuwa na mchango mkubwa katika benchi lake la ufundi.

“Anastahili kabisa kuwa sehemu ya timu yangu ya ufundi na ataleta mambo mengi mazuri katika nafasi yake kama mchambuzi,” amesema.

FOL 04

Mbali na sababu za kitaalamu, Folz pia ameeleza kuwa kumvuta Skudu Tunisia kuna maana kubwa kwake binafsi, kwani ni njia ya kuendelea kuwa karibu na Afrika Kusini, nchi ambayo anaipenda sana.

“Najua jinsi watu wanavyompenda nchini Afrika Kusini, nchi ambayo ninaipenda kwa moyo wangu wote. Kwa kuwa na Skudu, nina sehemu ndogo ya Afrika Kusini pamoja nami kila siku, na hilo ni jambo zuri,” amesema.

Skudu aliyewahi pia kucheza katika klabu kadhaa zikiwemo Orlando Pirates na Marumo Gallants za Afrika Kusini, sasa anaanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka akiwa upande wa benchi la ufundi baada ya kumaliza safari yake ya uchezaji.

Folz na Skudu ambao wote wamepita Yanga kwa nyakati tofauti, wawili hao walikutana Marumo Gallants msimu wa 2022-2023.

Folz alifundisha hapo kwa takribani miezi miwili kuanzia Julai 1, 2022 hadi Septemba 4, 2022, akaondoka na kumuacha Skudu hadi Julai 19, 2023 alipotua Yanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *