
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza mabadiliko ndani ya safu ya juu ya utumishi wa umma baada ya kufanya uteuzi na uhamisho wa manaibu makatibu wakuu katika ofisi na wizara mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Julai 22, 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yamegusa Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Pia, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika uteuzi huo, Dk Latifa Mohammed Khamis ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia masuala ya Muungano.
Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), nafasi aliyotumikia kwa kusimamia sera za ukuzaji biashara, masoko na uwekezaji.
Kuteuliwa kwake kunatazamwa kama kuhamisha uzoefu wake wa usimamizi wa taasisi kubwa za umma kwenda katika eneo nyeti la uratibu wa masuala ya Muungano, ambalo huhitaji uongozi wenye uwezo wa kuratibu taasisi na sekta mbalimbali za Serikali.
Vilevile, amemteua Ephraim Mafuru kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, akichukua nafasi hiyo baada ya kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Katika mabadiliko hayo pia, Prisca Lwangili ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
Rais Samia pia amemhamisha Abdallah Mitawi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Uchukuzi ambako sasa atahudumu kama Naibu Katibu Mkuu.
Mitawi ni miongoni mwa watendaji waliowahi kushiriki katika uratibu wa sera na shughuli za Serikali ndani ya Ofisi ya Makamu wa Rais, hivyo kuhamishiwa Wizara ya Uchukuzi kunatarajiwa kuongeza nguvu katika usimamizi wa sekta hiyo ambayo imeendelea kushuhudia uwekezaji mkubwa katika reli, bandari, viwanja vya ndege na usafiri wa majini.
Mabadiliko mengine yaliyofanywa ni kuhamishwa kwa Balozi Baraka Luvanda kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda Wizara ya Katiba na Sheria akiwa Naibu Katibu Mkuu.
Luvanda ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma na masuala ya uhusiano wa kimataifa.
Kupelekwa kwake katika Wizara ya Katiba na Sheria kunakuja wakati wizara hiyo inaendelea kusimamia maboresho mbalimbali ya sheria, haki na utawala bora pamoja na maandalizi ya masuala ya mabadiliko ya Katiba ambayo yanasubiri maridhiano ya kisiasa.
Aidha, Dk Franklin Rwezimula amehamishwa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambako atakuwa Naibu Katibu Mkuu.
Rwezimula ameendelea kujijengea sifa katika utendaji wa Serikali kupitia usimamizi wa masuala ya sheria na utawala, ambapo kuhamishiwa kwake Wizara ya Mambo ya Ndani kunamweka katika wizara inayosimamia vyombo vya usalama, uhamiaji, magereza, zimamoto na usajili wa watu, maeneo yanayohitaji uratibu wa karibu kati ya sheria na utekelezaji wa sera za Serikali.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Rais Samia amekuwa akifanya mabadiliko ya mara kwa mara katika safu ya viongozi waandamizi wa Serikali akisisitiza uwajibikaji, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Tofauti na mabadiliko yanayolenga kujaza nafasi zilizo wazi pekee, uteuzi huu mpya, umehusisha pia uhamisho wa watendaji kutoka sekta moja kwenda nyingine, wengi wao wakibadilishiwa wizara, jambo linaloonesha mkakati wa Serikali wa kutumia uzoefu wa viongozi katika maeneo mapya yenye mahitaji tofauti ya kiutendaji.
Aidha, katika mabadiliko hayo, Rais Samia amehamisha Dk Maduhu Kazi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mazingira.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu, uapisho wa naibu makatibu wakuu walioteuliwa utafanyika katika tarehe itakayopangwa baadaye.