Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kuweka msisitizo katika ufundishaji wa masomo ya dini shuleni, ikiwemo kugharamia vitabu vya masomo hayo, kama sehemu ya utekelezaji wa sera ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu inayozingatia imani yake.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema hayo leo Julai 22, 2026 wakati wa hafla ya kukabidhi vitabu vya somo la elimu ya dini ya Kiislamu kwa wanafunzi wa kidato cha sita ikiwa ni utekelezaji wa maboresho ya sera ya elimu.

Profesa Mkenda amesema Serikali imeweka kipaumbele katika masomo ya dini kwa kutambua mchango wake katika kujenga maadili na malezi ya wanafunzi.

“Serikali imeweka msisitizo sana kwenye masomo ya dini, ndiyo maana inagharamia vitabu na itaendelea kusisitiza watoto wanapokwenda shule wanapata mafundisho ya dini kulingana na imani zao,” amesema.

Amesema sera ya elimu inayotekelezwa sasa iliandaliwa kwa kushirikisha wataalamu pamoja na Watanzania wa imani mbalimbali ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya jamii.

“Sera hii ilipotengenezwa walikaa wataalamu na Watanzania wa imani zote walisikilizwa kujua wanataka nini,” amesema.

Profesa Mkenda ametoa wito kwa taasisi za dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuwekeza zaidi katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya shule.

“Tunaomba taasisi za dini ziendelee kutusaidia katika masuala ya elimu, hivyo tunawaomba muendelee kuwekeza kwenye elimu. Tuko tayari kukaa na wadau kuweka mikakati ya kuongeza nguvu kwa lengo la kuboresha shule na kujenga shule nyingine,” amesema.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kutekeleza sera ya elimu inayolenga kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa fursa ya kupata elimu kutokana na mazingira au sababu nyingine.

“Tutaendelea kutekeleza sera ya elimu na maelekezo ya Serikali kwamba asiachwe mtoto nyuma na fursa ya elimu. Tunajitahidi kutoa elimu kwa usawa. Fursa ya elimu imfikie kila mtoto wa Kitanzania bila ubaguzi,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Mufti wa Zanzibar, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar, Sheikh Siweid Ali Suweid amesema hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha ufundishaji wa masomo ya dini zimeondoa malalamiko yaliyokuwa yakitolewa na taasisi za dini kuhusu nafasi ya somo hilo katika mfumo wa elimu.

Amesema kwa sasa kuna ushirikiano mzuri kati ya Wizara ya Elimu, taasisi za elimu ya juu na Ofisi za Mufti wa Tanzania Bara na Zanzibar katika kuhakikisha masomo ya dini yanapewa uzito unaostahili.

“Tunashukuru kwa sasa Wizara imetulia, vyuo vimetulia, Ofisi ya Mufti wa Tanzania Bara na Zanzibar zimetulia. Tulikuwa tunapokea malalamiko mengi baada ya kutothaminiwa kwa somo la dini, lakini sasa tunaona limefanyiwa kazi na kwa sasa hakuna tatizo kwenye somo hilo,” amesema Sheikh Suweid.

Amesema hatua ya Serikali kugharamia vitabu vya elimu ya dini na kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji ni ishara ya kutambua mchango wa masomo hayo katika kujenga maadili, uzalendo na mshikamano miongoni mwa wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya Bakwata, Naibu Katibu Mkuu Utawala na Fedha wa baraza hilo, Mwenda Said Mwenda, ameipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua kurejesha na kuimarisha nafasi ya elimu ya dini katika mfumo wa elimu nchini, akisema maboresho ya Sera ya Elimu na mtaala mpya yameondoa malalamiko yaliyokuwapo kwa muda mrefu kuhusu kutothaminiwa kwa somo hilo.

Amesema Bakwata itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya elimu na kuunga mkono utekelezaji wa maboresho yanayolenga kuinua viwango vya elimu nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *