
Rais wa heshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ ameongoza mamia ya waombolezaji kwenye maziko ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo Iddi Kajuna.
MO ameshiriki katika shughuli hiyo ya maziko iliyofanyika kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam akiwa sambamba na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori.
Mbali na Dewji na Magori, Makamu wa Rais wa Yanga Arafat Haji naye ameshiriki maziko hayo sambamba na wadau mbalimbali wa klabu hiyo huku pia Makamu wa Rais wa Azam Abdulkarim Amin ‘Popat’ naye akiwa miongoni mwa waombolezaji.
Akizungumza baada ya maziko hayo, Arafat amesema Yanga imepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Kajuna na kwamba Simba wamepata pigo kwa kumpoteza kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele kuipigania.
“Nipo hapa kuiwakilisha klabu ya Yanga. Huu ni msiba mkubwa kwenye michezo hususan soka. Tukio kama hili linatuunganisha kama familia ya soka, upinzani wa klabu zetu tunaweka pembeni.
“Wakati tunapokea taarifa hii, Rais wangu (Hersi Said) alikuwa anaanza safari. Nikamwambia wewe nenda mimi nitakuja kushiriki msiba huu na watani wetu. Simba imepata pigo kubwa kwa kumpoteza Kajuna,” amesema Arafat.
Naye Popat amesema Kajuna alikuwa kiongozi mzuri, ambaye mara ya mwisho alikutana naye Pemba, kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo amewapa pole Simba kwa msiba huo.
“Tuko hapa kumsindikiza mwenzetu ambaye leo ametangulia na sisi tutafuata. Tumempoteza mwenzetu kwenye tasnia ya michezo hasa soka. Licha ya kwamba yeye (Kajuna) alikuwa Simba lakini sisi ni familia moja. Hivi karibuni binafsi nilikutana naye Pemba kwenye fainali. Tuliongea sasa unapopata taarifa kama hii lazima inashtua na kuumiza. Tunawapa pole wenzetu wa Simba kwa msiba huu,” amesema Popat