Dar es Salaam. Wakati hofu ikiendelea kutanda kuwa teknolojia ya Akili Unde (AI) inaweza kupunguza baadhi ya ajira za kawaida, wataalamu wa teknolojia wanasema mapinduzi hayo yamefungua wimbi la fursa za kazi zinazohitaji ujuzi wa kidijitali, uchambuzi wa taarifa na ubunifu, hali inayowapa vijana sababu mpya ya kuwekeza katika kujifunza teknolojia hiyo.
Kufuatia mapinduzi hayo, wataalamu hao wamewataka vijana kutokuiogopa AI bali kujifunza namna ya kuitumia kwa usahihi kuongeza thamani katika taaluma zao, wakisisitiza kuwa ajira za baadaye zitahitaji mchanganyiko wa ujuzi wa kidijitali, ubunifu, mawasiliano, uchambuzi na maadili kuliko uwezo wa kutumia kompyuta pekee.
Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Hafidh Mansour amesema maendeleo ya Akili Unde yamebadili aina ya ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Amesema kwa Tanzania, Akili Unde inaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana ikiwa mfumo wa elimu utaongeza mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia hiyo katika sekta mbalimbali.
“AI haiji kuchukua ajira zote kama wengi wanavyodhani. Badala yake imezalisha kazi mpya ambazo zinahitaji watu wenye uwezo wa kuisimamia, kuifundisha, kuichambua na kuitumia kutatua changamoto za taasisi na biashara,” amesema.
Amesema kampuni nyingi sasa zinatafuta wafanyakazi wanaoweza kuunganisha teknolojia na mahitaji ya biashara, jambo linalofungua fursa kwa vijana wenye ujuzi wa kidijitali.
Taaluma zitakazozalisha ajira
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, moja ya taaluma zinazokua kwa kasi ni Utaalamu wa kuandaa maelekezo ya AI (Prompt Engineering), ambayo inahusika na kuandaa maelekezo sahihi yanayoifanya AI kutoa majibu yenye ubora.
Amesema tofauti na dhana kwamba kutumia AI ni kuandika swali pekee, taaluma hiyo inahitaji uwezo wa kuchambua tatizo, kuelekeza mfumo na kupata matokeo yanayoweza kutumika katika biashara, elimu, utafiti na taasisi mbalimbali.
“Mtu mmoja anaweza kuuliza swali na kupata jibu la kawaida, lakini mtaalamu wa prompt engineering anaweza kupata uchambuzi wa kina unaoweza kutumika kufanya maamuzi,” amesema.
Amesema taaluma hiyo inaweza kufanywa na watu kutoka fani mbalimbali, wakiwemo waandishi wa habari, walimu, watafiti na wataalamu wa masoko.
Mtaalamu huyo amesema AI haiwezi kutoa majibu sahihi bila kuelekezwa kwa kutumia taarifa bora, jambo linalozalisha mahitaji ya wakufunzi wa mifumo ya AI.
Amesema wataalamu hao hukagua majibu yanayotolewa na AI, kurekebisha makosa na kuifundisha kuelewa lugha, tamaduni na mazingira mbalimbali.
“Kwa mfano, kama mfumo unatakiwa kuelewa Kiswahili vizuri, unahitaji watu wanaofahamu lugha hiyo kuufundisha sarufi, misemo na matumizi sahihi ya maneno,” amesema Mansour.
Ameongeza kuwa eneo hilo linaweza kuwapa nafasi walimu wa lugha, watafiti na waandishi kushiriki katika maendeleo ya AI inayozingatia mazingira ya Afrika Mashariki.
Kadri taasisi zinavyoendelea kukusanya taarifa nyingi, wataalamu wanasema mahitaji ya wachambuzi wa data yataendelea kuongezeka, kazi yao ikiwa ni kuchambua taarifa na kuzitafsiri ili kusaidia taasisi kufanya maamuzi sahihi.
“Data ndiyo mafuta yanayoendesha AI. Bila taarifa sahihi, hakuna mfumo wa AI unaoweza kufanya kazi vizuri. Sekta za afya, benki, kilimo, elimu na biashara tayari zinaongeza mahitaji ya wataalamu wa uchambuzi wa data,” amesema Mansour.
Mbali na hayo, Mtaalamu wa mifumo ya mtandao Jeremia Ngaiza amesema ukuaji wa matumizi ya Akili Unde pia umeongeza umuhimu wa wataalamu wa usalama wa mtandao.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, AI inaweza kutumiwa na wahalifu wa mtandao kutengeneza mashambulizi ya kidijitali, lakini pia inaweza kutumiwa kugundua na kuzuia mashambulizi hayo.
“Kadri matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya wataalamu wa kulinda taarifa za watu na taasisi yatakavyoongezeka,” amesema.
Ngaiza amesema kwenye sekta ya mawasiliano, akili unde imefungua nafasi kwa wabunifu wa maudhui wanaotumia teknolojia hiyo kuandaa maandishi, picha, video na sauti.
Hata hivyo, amesema ubunifu wa binadamu bado unabaki kuwa muhimu, akieleza kuwa Akili Unde inaweza kuandaa rasimu ya kazi, lakini ubunifu, maamuzi na maadili bado yanahitaji binadamu nyuma yake.
Mtaalamu huyo amesema matumizi ya AI katika afya, elimu, fedha na ajira yameongeza mahitaji ya wataalamu wa maadili ya teknolojia hiyo, watakaokuwa na jukumu la kuhakikisha mifumo yake inatumika kwa haki, inalinda taarifa binafsi na haibagui watumiaji.
“Tunahitaji watu watakaohakikisha AI inafanya maamuzi kwa haki na kutumia taarifa sahihi. Si kila jibu la AI linapaswa kukubalika bila kulichunguza,” amesema Ngaiza.
Akizungumzia upande wa biashara, Mansour amesema kampuni nyingi pia zitahitaji wasimamizi wa ujumuishaji wa AI watakaosaidia kuingiza teknolojia hiyo katika shughuli za kila siku.
Amesema wataalamu hao wataunganisha AI na mahitaji halisi ya biashara, ikiwemo kupanga usafirishaji, kuboresha huduma za benki, uchambuzi wa wagonjwa hospitalini na kuongeza ufanisi wa uzalishaji viwandani.
Kutokana na AI kuwa na uwezo wa kuzalisha taarifa nyingi kwa muda mfupi, Mansour amesema kutakuwa pia na uhitaji mkubwa wa wakaguzi wa taarifa za AI (AI Fact Checkers).
Amesema wataalamu hao watakuwa muhimu katika sekta ya habari, elimu, utafiti na serikali ili kuhakikisha taarifa zinazotolewa na AI ni sahihi na zinaweza kuaminika.
“Teknolojia inaweza kutoa taarifa zinazovutia lakini zenye makosa. Hivyo, kutakuwa na umuhimu mkubwa wa watu wenye uwezo wa kuhakiki na kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo,” amesema Mansour.