
Afrika inaweza kuongeza uchumi kwa asilimia 4
Utafiti mpya wa IMF unaonya kuwa iwapo kiwango cha sasa cha maandalizi hakitabadilika, katika kipindi cha miaka 10 AI itaongeza pato la eneo hilo kwa asilimia 0.2 pekee. Lakini nchi zikiweka mazingira yatakayoharakisha matumizi yake, mchango huo unaweza kufikia takribani asilimia 4.
Hatua hizo ni muhimu wakati Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ikitarajiwa kuwa na takribani nusu ya watu wote wapya watakaoingia katika soko la ajira duniani kufikia mwaka 2030.
IMF inaona AI kama nyenzo muhimu ya kuongeza tija, badala ya kuchukua nafasi za wafanyakazi.
IMF yaitaka Afrika kuwekeza katika umeme, intaneti na ujuzi
Ili kunufaika, IMF imetaka nchi za Afrika kuwekeza katika umeme wa uhakika, intaneti inayopatikana kwa watu wengi, miundombinu ya kuhimili takwimu (data) na kuwapatia wafanyakazi ujuzi wa kidijitali unaohitajika kutumia teknolojia mpya.
Serikali pia zimeshauriwa kuweka sheria zilizo wazi na zinazotekelezeka kuhusu matumizi na ulinzi wa data, ushindani, haki za watumiaji, usalama wa mtandao na matumizi yanayowajibika ya AI katika sekta ya umma.
AI itumike katika sekta muhimu za uchumi
Kwa mujibu wa IMF, teknolojia hiyo inapaswa kutumika kwa upana katika kilimo, elimu, afya, biashara ndogo ndogo na ukusanyaji wa kodi. AI inaweza kusaidia wakulima kufuatilia mazao, walimu kuwafikia wanafunzi, wahudumu wa afya kutambua na kufuatilia magonjwa, na wafanyabiashara kusimamia bidhaa na kufikia masoko ya nje.
Majaribio nchini Ghana, Nigeria, Rwanda na Uganda yanaonesha kuwa ushauri wa kidijitali unaweza kuongeza mapato, hasa unapounganishwa na pembejeo bora. Nchini Afrika Kusini, matumizi ya AI kufuatilia mazao yameonesha uwezo wa kuongeza uzalishaji na kupunguza upotevu wa chakula.
IMF imesisitiza kuwa AI barani Afrika si suala la teknolojia pekee, bali ni sehemu muhimu ya mkakati wa ukuaji wa uchumi. Manufaa yake yatapatikana ikiwa teknolojia hiyo itatumika kwa upana, kwa gharama nafuu na kwa usalama.