
Serikali, kampuni za teknolojia, wanazuoni na mashirika ya kiraia watatumia siku mbili katika Mdahalo wa Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI kujadili namna ya kudhibiti teknolojia ambayo inaendelea kwa kasi kuliko sheria zilizokusudiwa kuisimamia.
Iwapo itatumika kwa uwajibikaji, AI inaweza kuleta manufaa makubwa ya mabadiliko kwa watu duniani kote. Hata hivyo, pia kuna hofu kwamba teknolojia hii ya mapinduzi inazalisha hatari mpya. Na wakati AI inaendelea kukua kwa kasi ya ajabu, hatua za usimamizi zinazohitajika kuisimamia zinashindwa kwenda sambamba na maendeleo hayo.
Kabla ya mkutano huo, Idhaa ya Umoja wa Mataifa ilizungumza na washiriki wanne: wenyeviti wenza wawili wa Mdahalo wa Kimataifa na wenyeviti wenza wawili wa Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi la Umoja wa Mataifa kuhusu akili mnemba au AI, ambalo limechapisha ripoti kuhusu fursa na hatari za AI.
Walizungumzia manufaa ya AI, lakini pia hatari zake, pamoja na umuhimu wa kukubaliana kuhusu kanuni za msingi za kimataifa zinazokubalika na wote.
Yoshua Bengio ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa Jopo la UN la Kisayansi anasema: AI inakaribia kufikia au hata kuzidi uwezo wa binadamu katika nyanja nyingi. Inaendelea kwa kasi kuliko uelewa wa kisayansi na uwezo wa serikali kuendana nayo. Kumekuwa na maendeleo makubwa sana yanayobadilisha dunia, na hakuna dalili kwamba kasi hiyo itapungua.
Balozi Rein Tammsaar, Mwakilishi wa Kudumu wa Estonia kwenye UN na Mwenyekiti Mwenza wa Mdahalo wa Kimataifa: Kwa nchi nyingi duniani, AI inaweza kuwa chombo cha kuleta usawa wa fursa. Inaweza kusaidia maendeleo ya uchumi, kuongeza ushindani, kuimarisha sayansi na mifumo ya afya. Kujifunza kwa mashine kwa ujumla kunaweza kuongeza uzalishaji. Huo ndio uwezo wake.
Balozi Egriselda López , Mwakilishi wa Kudumu wa El Salvador kwenye UN na Mwenyekiti Mwenza wa Mdahalo wa Kimataifa: AI inaweza kuwa nyenzo kwa serikali kuboresha utendaji wake na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Balozi Tammsaar: AI ni nyenzo ambayo mamilioni ya watu duniani wanaweza kunufaika nayo. Lakini wakati huo huo, ikiingia mikononi mwa watu wenye nia mbaya, inaweza kutumiwa kwa madhumuni ya kulazimisha, kudhoofisha imani kwa serikali, kuvuruga mifumo ya kidemokrasia, kuendesha propaganda na kuhatarisha uadilifu wa taarifa.
Maria Ressa, Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la Kisayansi: Kizazi cha kwanza cha AI kilitumika katika mitandao ya kijamii, na kilifanya uongo usambae kwa kasi zaidi. Ujumbe uliojaa hofu, hasira na chuki husambaa kwa kasi kubwa. Uadilifu wa taarifa ndiyo kiini cha mapambano haya. Usipoweza kutofautisha ukweli na uongo, huwezi kuwa na demokrasia.
Hii ndiyo changamoto tunayokabiliana nayo, na ndiyo sababu ninaiita kuporomoka kwa ukweli na kuaminiana kwenye zam za kidijitali au ‘information Armageddon’.
Yoshua Bengio: Kadiri ushahidi wa AI kuonesha tabia za udanganyifu unavyozidi kuongezeka, sayansi kwa sasa haiwezi kuthibitisha kwamba uwezo wake utakapoendelea kuongezeka, haitasababisha madhara ya janga, iwe kwa kujitegemea au kupitia watumiaji wenye nia ovu.
Balozi Tammsaar: Waendelezaji wakuu wa AI wamejikita katika nchi mbili tu [Marekani na China]. Hali hii inaziacha nchi nyingine zikiwa na maswali mengi.
Nchi zinazoendelea, hasa, zina hofu kwamba katika hali mbaya zaidi, pengo la AI litaziacha nyuma. Teknolojia hii inaendelea kwa kasi kiasi kwamba huenda zisipate nafasi ya kufidia pengo hilo na kuendana na maendeleo.
Balozi López: Pengo la AI ni la kweli. Baadhi ya nchi zina miundombinu imara, wataalamu wenye ujuzi mkubwa na uwezo mkubwa wa kufanya utafiti. Nyingine bado zinakabiliwa na changamoto za msingi kama vile upatikanaji wa intaneti na miundombinu ya umma.
Maria Ressa: Dunia haiwezi kusimamia kile ambacho haikielewi. Ripoti ya Jopo inatoa maarifa huru ya kisayansi yaliyotolewa na wataalamu kutoka kila eneo la dunia na yanayopatikana kwa kila serikali. Ujumbe wake uko wazi: uwezo wa AI ni mkubwa, lakini hatari zake ni halisi, na gharama ya kuchelewa kuchukua hatua inaongezeka.
Yoshua Bengio: Ningependa serikali nyingi zaidi duniani zielewe mwelekeo unaowezekana wa maendeleo ya AI katika siku zijazo. Hatuna mifumo sahihi ya usimamizi katika ngazi ya kitaifa wala ya kimataifa, na pia hatuna njia bora za kuhakikisha manufaa yake yanagawiwa kwa watu wote. Ili kuchukua hatua kwa ufanisi, watunga sera wa dunia lazima waelewe mifumo hii.
Balozi López: Mdahalo wa Kimataifa ni jukwaa la kwanza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kujadili usimamizi wa AI. Pia ni fursa kwa nchi wanachama kukutana na kufanya majadiliano jumuishi. Sio serikali pekee zinazohusika, bali pia wadau mbalimbali.
Maria Ressa: Hakuna nchi hata moja inayoweza kushughulikia teknolojia hii peke yake. Inahitaji suluhisho la ushirikiano wa kimataifa. Chombo kilicho katika nafasi nzuri ya kufanya hivyo ni Umoja wa Mataifa. Swali sasa ni: je, nchi wanachama wake zitachukua hatua?
Umoja wa Mataifa na AI
Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu akili mnemba linaundwa na wataalamu 40 kutoka nchi 36, wanaohudumu kwa uwezo wao binafsi. Jopo hilo lilichapisha ripoti yake ya kwanza tarehe 1 Julai.
Kazi ya Jopo hilo inachangia Mdahalo wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usimamizi wa AI ulioanza leo na utamalizika kesho Julai 7.