s

Chanzo cha picha, Screengrab

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 2

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kuendelea kudai kupatikana kwa Katiba mpya yenye maridhiano ya kitaifa, akisema ndiyo msingi wa kuimarisha haki za binadamu, utawala bora na demokrasia nchini.

Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) jijini Dar es Salaam Ijumaa, Dkt Nchimbi alisema kama angepewa nafasi ya kuwaambia Watanzania jambo moja tu, angewaambia: “Pambaneni mpate Katiba mpya.”

Kauli hiyo inakuja wakati mjadala kuhusu Katiba mpya ukiendelea nchini Tanzania. Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulianza mwaka 2011 chini ya Rais Jakaya Kikwete lakini ukakwama mwaka 2014 kabla ya kupigiwa kura ya maoni. Rais Samia Suluhu Hassan amesema mchakato huo utafufuliwa kabla ya mwaka 2030, huku Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya uchaguzi wa mwaka 2025 pia ikiahidi kuendeleza mchakato huo.

“Pambaneni mpate Katiba ambayo ina makubaliano ya wadau wote, Katiba yenye muafaka katika taifa, Katiba itakayotupeleka mbele miaka 50 inayokuja na ambayo kila Mtanzania atajivunia kwa sababu inajali maisha ya mtu na kuheshimu haki za raia wake,” alisema.

Makamu wa Rais alisema haki za binadamu si suala la sheria pekee bali zinagusa maisha ya kila siku ya kila Mtanzania.

“Haki ni mama anayetaka mtoto wake awe salama, ni baba anayetaka kulisha familia yake kwa heshima, ni kijana anayetaka kusikilizwa, ni mwananchi anayetaka kutoa maoni yake bila hofu, ni mtuhumiwa anayestahili kutendewa kwa mujibu wa sheria, ni polisi anayekwenda kazini akitarajia kurudi salama kwa familia yake na ni mwandishi wa habari anayetaka kufanya kazi yake. Hata kama hana cheo, hana fedha wala mtu wa kumsemea, bado ana utu na kwa sababu ana utu ana thamani. Hapo ndipo haki za binadamu zinapoanzia,” alisema.

Alisema ingawa wananchi na makundi mbalimbali huwasilisha madai mengi kwa wakati mmoja, msingi wa kuyatatua ni kuwa na Katiba inayokubalika na wote.

“Ukisikiliza madai mengi ya watu mbalimbali, unakuta wamepanga mambo mengi kwa wakati mmoja. Lazima uchague jambo kubwa linaloweza kubeba yote katika nchi. Ni Katiba,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya THRDC, Pili Mtambalike, alisema maridhiano ya kitaifa, mshikamano na umoja ni msingi wa kujenga taifa lenye amani na maendeleo endelevu.

Alisema maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira yanayolinda haki za binadamu na yanayowapa wananchi nafasi ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

Mtambalike aliongeza kuwa maridhiano ni daraja la kuliponya taifa, kujenga utulivu na kutatua tofauti kupitia mazungumzo badala ya migawanyiko.

Kuhusu Katiba nmpya pia mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai pamoja na Tume ya Jaji Chande zilizoundwa na Rais, yanaonesha umuhimu wa kuendelea na mchakato wa Katiba mpya ili kuimarisha utawala bora, demokrasia na ulinzi wa haki za binadamu nchini.

Kwa miaka mingi, wanaharakati, vyama vya upinzani na baadhi ya wananchi wameendelea kushinikiza kupatikana kwa Katiba mpya kutoka inayotumika sasa ya mwaka 1977, wakisema itasaidia kuimarisha uwajibikaji, demokrasia na ulinzi wa haki za binadamu, ingawa kumekuwa na mitazamo tofauti kuhusu namna na wakati wa kuendelea na mchakato huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *