• Mike Sonko amesema urafiki wake na rais mstaafu Uhuru Kenyatta ulianza kuzorota kutokana na mradi wa Northlands City, wakati matatizo ya mifereji ya maji katika Kaunti ya Kiambu yalipotishia kuathiri Nairobi
  • Anadai alishinikizwa kuunga mkono ubomoaji wa makazi katika eneo la Ruai ili kupisha mfumo wa kupitisha maji taka wa mradi huo, lakini alikataa kwa kuhofia hatua hiyo ingeharibu mustakabali wake wa kisiasa
  • Sonko amesema kukataa kwake kulifungua njia kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Nairobi Metropolitan Services (NMS), Mohamed Badi, kusimamia shughuli za ubomoaji

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko amefunguka kuhusu chanzo cha mzozo uliovuruga urafiki wake wa karibu na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema tofauti zao zilianza kutokana na mradi wa mabilioni ya shilingi wa Northlands City.

Rais wa zamani Uhuru Kenyatta akiwa na Mike Sonko.
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko akiwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika hafla ya awali. Picha: Mike Sonko.
Source: Facebook

Northlands City ni mradi unaoungwa mkono na familia ya Kenyatta unaoenea katika ekari 11,576 mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu, takriban kilomita 15 kutoka Nairobi.

Mradi huo wenye thamani ya takribani KSh bilioni 500 umepangwa kuhudumia wakazi wapatao 250,000 katika kipindi cha miaka 50, ukijumuisha maeneo ya makazi, bustani za viwanda, vituo vya biashara, maeneo ya burudani, ardhi ya uhifadhi, maeneo ya kilimo pamoja na uwanja binafsi wa ndege.

Pia soma

Maoni Mseto huku Matiang’i akikutana na Sifuna siku moja baada ya Pauline Njoroge kuondoka Jubilee

Akizungumza katika Spice FM Alhamisi, Julai 24, Sonko alisema matatizo yalianza wakati ukubwa wa mradi wa Northlands pamoja na maendeleo mengine yaliyoibuka katika maeneo ya kifahari ya Kiambu ulipozidi uwezo wa mifereji ya maji wa eneo hilo, na hivyo kulazimu wapangaji kutafuta suluhisho kupitia miundombinu ya Nairobi.

“Kulikuwa na uwekezaji huu wa Northlands. Ulikuwa uwekezaji mzuri pamoja na maeneo mengine ya makazi yaliyokuwa yakiibuka katika maeneo hayo ya kifahari. Hakukuwa na mifereji ya kutosha kuhimili uwekezaji na maendeleo hayo. Mifereji ya Kiambu haikuwa ya kutosha, haikuweza kubeba maji taka,” Sonko alisema.

Alieleza kuwa suluhisho lililopendekezwa lilikuwa kupitisha maji taka kupitia mfumo wa mifereji wa Nairobi hadi Ruai, hatua ambayo ingehitaji serikali ya kitaifa na serikali ya Kaunti ya Nairobi kuwahamisha zaidi ya watu milioni moja waliokuwa wakiishi katika makazi yasiyo rasmi.

“Kwa hiyo ikaamuliwa tutumie mifereji ya Nairobi kupeleka maji taka hadi Ruai. Kufanya hivyo kulimaanisha serikali ya kitaifa na serikali ya Kaunti ya Nairobi zingelazimika kuwahamisha zaidi ya wakazi milioni moja wa mabanda,” alisema.

Sonko alifichua kuwa alielekezwa kushirikiana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Karanja Kibicho kupanga ubomoaji wa makazi hayo ili kupisha mradi wa mifereji, lakini alikataa kutekeleza agizo hilo.

Pia soma

Magazeti ya Kenya: Jinsi mashine ya kampeni ya Gachagua iIlivyoleta ushindi mkubwa wa 85% Ol Kalou

“Niliambiwa nikutane na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i na Katibu Mkuu Karanja Kibicho ili kutafuta njia za kubomoa mabanda na kuwahamisha wakazi wake ili mifereji ipite. Nilitofautiana na Matiang’i, Kibicho na timu ya usalama ya taifa kwa sababu bado nilikuwa na mustakabali wa kisiasa nchini,” alisema.

Video; kwa hisani

Aliyekuwa gavana huyo, ambaye alikuwa akihudumu muhula wake wa kwanza wakati huo, alisema kusita kwake kulitokana na hofu ya kuharibu maisha yake ya kisiasa, akibainisha kuwa Uhuru, aliyekuwa katika muhula wake wa mwisho wa urais, hakuwa tena na presha ya kutafuta kura.

“Huo ulikuwa muhula wangu wa kwanza kama gavana. Rais alikuwa anaelekea kustaafu, hakujali. Nilikataa kwenda na askari wa kaunti kuwapiga na kuwafukuza watu walioniweka madarakani,” Sonko alisema.

Alisema kukataa kwake kulisababisha kuletwa kwa Luteni Jenerali Mstaafu Mohamed Badi, ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa iliyokuwa Nairobi Metropolitan Services (NMS), ili kusimamia ubomoaji huo badala yake.

“Kisha wakamleta mwanajeshi aje afanye kazi hiyo. Tulitengwa kwa sababu hatukufuata kile bosi (Uhuru) alitaka,” Sonko alisema.

Ubomoaji uliofanywa wakati wa uongozi wa NMS miaka iliyopita ulilenga majengo yaliyokuwa kwenye maeneo ya kingo za mito na njia za mifereji ya maji jijini Nairobi, hatua iliyokosolewa na wakazi walioathirika pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu wakati huo.

Pia soma

Mwanaume wa Kakamega aliyefungwa jela miaka 20 baada ya kumtuma bintiye jirani dukani afungua roho

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *