KLABU ya Simba, imeinasa saini ya mshambuliaji, Ibrahim Doumbia kutoka AS Korofina ya Mali kwa mkataba wa miaka miwili.
Doumbia (19) raia wa Mali, ni mshambuliaji kijana anayetajwa kuwa mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa aina zote akitokea sehemu yoyote uwanjani.
Rekodi zinaonesha, msimu uliopita akiwa na AS Korofina, Doumbia ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Mali akifunga mabao 17 na kusaidia kupatikana kwa mengine matano.
Doumbia ambaye pia amejumuishwa pia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Mali chini ya umri wa miaka 20, amefunga mabao 22 katika michuano yote baada ya kucheza mechi 26.
Taarifa ya Klabu ya Simba, imesema: “Tumefanikiwa kuinasa saini ya mshambuliaji, Ibrahim Doumbia kutoka AS Korofina ya Mali kwa mkataba wa miaka miwili.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri kwenye michuano ya ndani pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na usajili tunaoufanya unazingatia matakwa hayo.”
Akizungumza kuhusu mipango ya msimu ujao, kocha wa Simba, Steve Barker, amesema moja ya maeneo ambayo yeye na uongozi wa klabu walikubaliana kuyaimarisha katika dirisha hili la usajili ni nafasi ya mshambuliaji wa kati.
“Baada ya tathmini ya msimu tulikubaliana kuwa tunahitaji kuongeza ubora katika baadhi ya maeneo. Moja ya nafasi hizo ni mshambuliaji wa kati ili kuongeza ushindani na kuwa na chaguo zaidi ndani ya kikosi,” amesema Barker.
Kauli hiyo imeendana na harakati zilizofanywa na Simba za kumsajili Doumbia ambaye pia ilielezwa alitolewa macho na klabu za Afrika Kusini.
Akizungumza na Mwanaspoti, mchambuzi wa soka wa Mali, Mamadou Sidibé, amesema Doumbia ni mshambuliaji anayejitofautisha kwa uwezo wake wa kusoma mchezo na kutengeneza nafasi hata akiwa hana mpira.
“Doumbia ni mshambuliaji anayejua kusoma mchezo vizuri, mikimbio yake bila mpira huwafanya mabeki washindwe kujipanga na mara nyingi humkuta akiwa katika nafasi sahihi ya kufunga,” amesema Sidibé.
Mchambuzi huyo amesema silaha nyingine ya mshambuliaji huyo ni utulivu wake anapokuwa ndani ya eneo la hatari, akieleza kuwa hutumia nafasi chache kupata mabao.
“Ni mchezaji mwenye utulivu mkubwa kwenye umaliziaji, ana uwezo wa kufunga kwa miguu yote miwili na pia ni mzuri kwenye mipira ya juu,” amesema.
Kwa mujibu wa Sidibé, Doumbia pia anafahamika kwa uwezo wake wa kuanzisha presha kwa mabeki wa wapinzani, jambo linalosaidia timu yake kurejesha umiliki wa mpira haraka.
“Anapenda kukaba kuanzia mbele. Hiyo ni sifa ambayo kila kocha anayependa mpira wa kasi huifurahia kwa mshambuliaji wake,” amesema.
Mahitaji ya Simba ya kupata mshambuliaji mpya yalionekana wazi mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kukumbwa na changamoto katika eneo hilo.
Kusimamishwa kwa Jonathan Sowah kulilazimisha benchi la ufundi kumtumia kiungo mshambuliaji, Elie Mpanzu kucheza kama mshambuliaji wa kati katika baadhi ya mechi muhimu za mwisho wa msimu ili kuziba pengo lililoachwa.
Sowah tayari amerejea Singida Black Stars baada ya kuachana na Simba, hali iliyoongeza umuhimu wa klabu hiyo kutafuta mshambuliaji mwingine wa asili kabla ya kuanza kwa msimu wa 2026-2027.
Doumbia ni mchezaji wa kwanza mpya wa kimataifa kutambulishwa Simba kuelekea msimu ujao, huku akiwa wanne kwa ujumla baada ya Kelvin Nashon, Nathaniel Chilambo na Bakari Msimu.