
Kagera Sugar imekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa maafande wa Polisi Tanzania, Naku James Kazimoto kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya kushindwa kufikia makubaliano na waajiri wake ya kuongeza upya kandarasi nyingine.
Nyota huyo aliyeiwezesha Polisi Tanzania kurejea Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, amejiunga na kikosi hicho ambacho pia kitashiriki Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, kikiungana na mabingwa wa Ligi ya Championship timu ya Geita Gold.
Akizungumza na Mwanaspoti, Naku amesema zipo ofa mbalimbali ila bado hajafikia makubaliano na timu yoyote kwa ajili ya kujiunga nayo kwa msimu ujao, japo hatokuwa sehemu ya kikosi cha Polisi Tanzania baada ya kutoongeza tena mkataba mpya.
“Ni kweli nimeondoka Polisi Tanzania baada ya mkataba wangu kuisha, tulikuwa katika mazungumzo lakini tumeshindwana na nimeamua kutafuta changamoto sehemu nyingine, muda sio mrefu nitaweka wazi timu nitakayojiunga nayo,” amesema Kazimoto.
Nyota huyo aliyefunga mabao manne kwa msimu wa 2025-2026, katika Championship, kabla ya kujiunga na Polisi alikuwa Mbuni FC ya jijini, Arusha, ambayo kwa msimu wa 2024-2025, alimaliza kinara ndani ya kikosi hicho baada ya kufunga mabao 12.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Mbuni FC katika dirisha dogo la Januari 2024, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Copco FC cha jijini, Mwanza na msimu wa 2023-2024, aliifungia timu hiyo ya Arusha mabao 10, ya Championship.