Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian ameipa wiki mbili timu ya wataalamu aliyoiunda kuchambua maoni ya wadau mbalimbali na kuwasilisha mapendekezo yatakayosaidia kupata suluhu ya matumizi ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange, kilichozua mjadala kutokana na kuchelewa kuanza kutumika kikamilifu.

Dk Burian ametoa maelekezo hayo leo Jumamosi, Julai 25, 2026, baada ya kikao kilichowakutanisha wadau wa sekta ya usafirishaji, viongozi wa Serikali, Mbunge wa Jimbo la Tanga na wananchi kujadili mustakabali wa kituo hicho.

Amesema timu hiyo, inayoundwa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Tanga, imepewa jukumu la kuchakata maoni yote yaliyotolewa na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa katika kikao kingine kitakachofanyika baada ya wiki mbili.

“Timu ya wataalamu iliyokuwa ikiandika maoni haya tunaipa muda wa kuyachakata. Baada ya wiki mbili tutakutana tena kujadili mapendekezo hayo na kuamua njia bora ya kuhakikisha Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange kinatoa huduma stahiki kwa wananchi,” amesema Dk Burian.

Kikao hicho kimekuja kufuatia mgogoro ulioibuka baada ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kushindwa kutekeleza mpango wake wa kuanzia Julai 15, 2026 wa kuyahamishia mabasi yote yanayofanya safari za mikoani katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange.

Baada ya mpango huo kukwama, Meya wa Jiji la Tanga, Mustapher Mhina maarufu Selebosi, alisema si busara kuendelea kuacha kituo hicho pamoja na jengo la kitega uchumi lililojengwa kwa fedha za Serikali vikibaki bila kutumika.

Alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Fedha ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Tanga ilipendekeza kituo hicho kibadilishiwe matumizi na kitumike kama eneo la maegesho ya malori.

Hata hivyo, viongozi wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Wadogo Tanzania (JWT), walieleza kuwa wamiliki wa mabasi hawajakataa kutumia Kituo cha Kange, bali walikuwa wakisubiri kufanyika kwa maboresho waliyoainisha.

Walisema miongoni mwa mapendekezo yao ni kupewa muda wa miezi sita ili Serikali ikamilishe maboresho ya miundombinu katika kituo hicho, huku wao wakijenga kituo cha kupakia na kushusha abiria katikati ya Jiji la Tanga ili kupunguza msongamano katika barabara za 12, 13 na 14.

Katika kikao hicho, wadau mbalimbali wa usafirishaji wamesisitiza kuwa hawapo tayari kuona kituo hicho kikibadilishwa matumizi, wakieleza kuwa kilijengwa kwa lengo mahsusi la kuhudumia mabasi ya masafa marefu.

Mbunge wa Jimbo la Tanga, Kassim Mbarouk (Makubel), amesema eneo la Kange lilichaguliwa kwa kuzingatia upanuzi wa Jiji la Tanga na kwamba kadri mji unavyoendelea kukua pamoja na ujenzi wa barabara mpya, kituo hicho kitakuwa sehemu muhimu ya kitovu cha shughuli za usafiri.

Amewataka wadau wa usafirishaji kuondoa hofu kuhusu matumizi ya kituo hicho na badala yake kushirikiana na Halmashauri ili kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha huduma kwa wananchi.

Naye mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Ratco, Mohamed Salim, ameiomba Halmashauri ya Jiji la Tanga kushirikiana na wamiliki wa mabasi badala ya kuweka mazingira yanayoweza kukwamisha shughuli zao.

Amesema sekta ya usafiri wa mabasi ina mchango mkubwa katika kuwahudumia wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi, hivyo maamuzi yanayofanywa yanapaswa kuzingatia maslahi ya wadau wote.

Kituo Kikuu cha Mabasi cha Kange kilianza kujengwa mwaka 2012 na kukamilika mwaka 2014 kwa gharama ya takribani Sh6.8 bilioni kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TSCP).

Aidha, jengo la kitega uchumi lililopo katika eneo hilo lilijengwa kati ya mwaka 2019 na 2023 kwa gharama ya Sh8.76 bilioni kutoka Serikali Kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *