
Kuishi muda mrefu duniani hakumaanishi kuongeza idadi ya miaka pekee, bali kuongeza miaka ambayo mtu anaishi akiwa na afya njema, uwezo wa kufanya shughuli zake kwa uhuru na kujumuika na jamii yake.
Jambo hili huwa mada ya msingi hasa kwa watu wenye umri unaokaribia uzee, wengi hujiuliza nini wanapaswa kufanya ili maisha yao hasa ya uzee yawe marefu na bila matatizo ya kiafya yanayotokana na uzee huo.
Wakati mazoezi ya viungo, matumizi sahihi ya dawa na ulaji bora yakitawala mjadala huo miongoni mwa wataalamu wa afya, Dk David Barzilai, daktari wa tiba ya maisha marefu (longevity medicine physician) kutoka Marekani, anataja mambo matano muhimu yanayoweza kumpa mtu nafasi ya kuishi maisha marefu akiwa na afya imara.
Katika chapisho la Pathways to Longevity lililochapishwa na Harvard Health Publishing mwaka 2026, Dk Barzilai anasema watu wengi hawatamani kuongezewa miaka ya kuishi wakiwa dhaifu na tegemezi, bali wanataka miaka zaidi wakiwa na afya njema, wakitembea kwa uhuru, wakifikiri vizuri na wakiendelea kushiriki katika kazi na uhusiano wanaouthamini.
Anasema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la utafiti na shauku kuhusu maisha marefu yenye afya kutokana na maendeleo ya kisayansi yanayoonesha umuhimu wa mtindo wa maisha katika kuamua ubora wa uzee.
Kwa mujibu wa Dk Barzilai, ingawa vinasaba vina mchango katika kuishi muda mrefu na kubaki na afya, mtindo wa maisha una nafasi kubwa pia.
Nchini Tanzania, kwa mujibu wa takwimu za Serikali zilizotumika katika Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2024, wastani wa umri wa kuishi umeongezeka hadi miaka 66.2 kutoka miaka 52.6 mwaka 2003.
Ongezeko la idadi ya wazee limeongeza umuhimu wa kuhakikisha miaka hiyo inaambatana na afya bora, uwezo wa kujitegemea na ushiriki katika jamii.
Dk Barzilai anataja mambo matano yanayojitokeza mara kwa mara katika tafiti za maisha marefu akisisitiza kuwa yakizingatiwa kikamilifu ipo nafasi ya kuishi uzee wenye afya.
“Afya bora haina siri za ajabu. Kinachohusika zaidi ni mambo ya msingi ambayo watu wengi tayari wanayajua, lakini mara nyingi hushindwa kuyafanya kwa uendelevu kwa miongo mingi,” anasema Dk Barzilai.
Mazoezi ya mwili
Akizungumzia umuhimu wa mwili kuwa katika harakati, Dk Barzilai anasema kufanya mazoezi ni miongoni mwa mambo yenye athari kubwa kwa mifumo mingi ya mwili kwa wakati mmoja.
Anasema mazoezi huboresha uwezo wa mwili kutumia insulini, afya ya ubongo, uimara wa mifupa na uwezo wa moyo pamoja na mapafu kufanya kazi vizuri.
Anashauri kuchanganya aina mbalimbali za mazoezi, ikiwemo mazoezi ya kuimarisha misuli mara mbili kwa wiki na kufanya dakika 150 za mazoezi ya wastani au dakika 75 za mazoezi makali kila wiki.
Pia, anasema hata shughuli ndogo za kila siku zina umuhimu, akieleza kuwa kuvunja muda mrefu wa kukaa kwa kufanya kazi nyepesi kwa dakika chache kunaweza kusaidia kuboresha kiwango cha sukari kwenye damu na shinikizo la damu.
Lishe bora
Katika jambo la pili, Dk Barzilai anasema chakula kina mchango mkubwa katika mazingira ambayo seli za mwili huishi kila siku, kwa kuathiri kiwango cha sukari kwenye damu, uchochezi mwilini na uwezo wa mwili kujenga misuli na kujirekebisha.
Anashauri watu kutumia vyakula halisi, kupata protini ya kutosha ambayo umuhimu wake huongezeka kadri mtu anavyozeeka, pamoja na kuepuka ongezeko kubwa la sukari kwenye damu linaloweza kusababishwa na kula zaidi wanga uliokobolewa.
Anasema milo inapaswa kuhusisha protini, mafuta yenye afya na vyakula vyenye nyuzinyuzi.
Usingizi wa kutosha
Kwa mujibu wa Dk Barzilai, usingizi ni msingi muhimu wa maisha marefu kwa sababu mwili hutumia muda huo kufanya kazi za kujirekebisha.
Anasema wakati wa usingizi, mwili huondoa taka za kimetaboli kwenye ubongo, kuimarisha kumbukumbu na kurekebisha homoni zinazodhibiti hamu ya kula pamoja na msongo wa mawazo.
Aidha, wataalamu wengi pia wanashauri watu wazima kulala saa saba hadi nane kila usiku. Katika hilo, Barzilai anasisitiza kwamba kuwa na ratiba thabiti ya kulala na kuamka ni jambo muhimu kwa afya bora
Kudhibiti msongo wa mawazo
Dk Barzilai anasema msongo wa mawazo wa muda mfupi unaweza kuwa na faida kwa sababu husaidia mwili kukabiliana na changamoto, lakini tatizo hutokea pale unapokuwa wa kudumu.
Anasema msongo wa muda mrefu unaweza kuathiri mfumo wa moyo na mishipa ya damu, kinga ya mwili, usingizi na mfumo wa kimetaboli, hali inayoweza kuharakisha baadhi ya michakato ya kuzeeka.
Anashauri njia bora za kudhibiti msongo kuwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kupata usingizi wa kutosha, kupata mwanga wa asili na kutumia muda na watu wanaoaminika.
Uhusiano wa kijamii
Akizungumzia nguzo ambayo haitajwi mara nyingi, Dk Barzilai anasema uhusiano wa kijamii ni sehemu muhimu ya maisha marefu ambayo watu wengi hawaipi uzito unaostahili.
Anasema watu wengi hufuatilia kwa karibu chakula wanachokula na idadi ya hatua wanazotembea kila siku, lakini hawatengi muda sawa katika kulinda urafiki na uhusiano wao, licha ya ushahidi kuonyesha umuhimu wake kwa afya.
Anashauri watu wanaojisikia wapweke kuanza na hatua ndogo, kama kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na mtu wanayemwamini, kushiriki shughuli za kijamii au kujitolea zinazowaunganisha na watu wengine.
Hata hivyo, anasema uhusiano wa kijamii ndiyo nguzo inayopuuzwa zaidi huku usingizi, shughuli za mwili na lishe bora zikiwa msingi wa afya ya kila siku.
Mtaalamu huyo anahitimisha kuwa badala ya kutafuta njia za miujiza za kuongeza umri wa kuishi, mtu anapaswa kutambua eneo ambalo ana udhaifu mkubwa na kuanza kuboresha eneo hilo kwa sababu ndilo linaweza kuleta mabadiliko zaidi katika afya yake.