Babati. Wakulima wa mazao ya jamii ya mikunde nchini wanatarajiwa kunufaika na mfumo mpya wa kidijitali utakaowaunganisha na wanunuzi, wafanyabiashara na wadau wa sekta hiyo, huku ukiwawezesha kupata taarifa za bei za mazao na masoko kwa wakati.
Mfumo huo umezinduliwa leo Jumamosi, Julai 25, 2026 mjini Babati, Mkoani Manyara ukiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi za masoko, bei za mazao na fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mikunde.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mratibu wa Mtandao wa Mfumo wa Kidijitali wa Mazao ya Jamii ya Mikunde Tanzania, Zirack Andrew amesema mfumo huo utaleta mabadiliko makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara kwa kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi ya biashara.
Amesema kupitia mfumo huo, wadau wataweza kufahamu bei za mazao kwa wakati, kupata taarifa mbalimbali za kilimo na kuunganishwa na masoko yenye uhakika.
“Mfumo huu utarahisisha kuwaunganisha wadau wote katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mikunde, kuimarisha ushirikiano wao, kukuza biashara na kuongeza kipato cha wakulima,” amesema Andrew.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Alizeti Tanzania, ambaye pia ni mfanyabiashara wa mazao, Athuman Karunde, amesema matumizi ya mfumo huo yataongeza upatikanaji wa mazao yenye ubora na kujenga uaminifu kati ya wakulima na wanunuzi.
Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa mazao ya jamii ya mikunde uliofanyika wilayani Babati, mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuboresha biashara ya mazao ya kilimo kwa kuweka mazingira ya uwazi katika upatikanaji wa taarifa za masoko.
Mrajisi Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, amesema teknolojia hiyo ni fursa muhimu kwa wakulima kupata masoko ya uhakika na kuongeza thamani ya mazao yao.
“Matumizi ya mfumo huu wa kidijitali yatawasaidia wakulima kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia,” amesema Merinyo.
Baadhi ya wakulima walioshiriki uzinduzi huo wamesema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo walikuwa wakikosa taarifa sahihi za masoko, hali iliyowalazimu kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ya chini.
Mkulima kutoka Katesh AMCOS wilayani Hanang’, Elizabeth Mfuko, amesema ana matumaini mfumo huo utamwezesha kupata bei za ushindani na kuondoa utegemezi kwa wanunuzi wa kati.
“Mfumo huu wa kidijitali utatusaidia kuondokana na walanguzi ambao wamekuwa wakitununulia mazao kwa bei ya chini, kwa sababu tutakuwa tunaona bei halisi za soko kupitia mtandao,” amesema.
Naye mkulima kutoka Gendi AMCOS wilayani Babati, Naai Bernald, amesema mfumo huo utawarahisishia kufuatilia taarifa mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mikunde kwa njia ya kidijitali.
“Dunia imebadilika, taarifa nyingi sasa zinapatikana kupitia teknolojia. Tunashukuru kupata fursa hii ambayo itatusaidia kufanya biashara kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Wadau wa sekta ya kilimo wanaamini matumizi ya mfumo huo yataongeza uwazi katika biashara ya mazao ya mikunde, kuboresha upatikanaji wa masoko na kuongeza kipato cha wakulima nchini.