ALIYEKUWA mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Kassim Shaibu ‘Mayele’ amekamilisha usajili wake wa kujiunga na TRA United kwa mkataba wa miaka miwili, baada ya mabosi wa kikosi hicho kuvutiwa na kiwango bora cha mchezaji huyo msimu wa 2025-2026.

Mshambuliaji huyo amekamilisha usajili huo na kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na Mtibwa Sugar ambayo tayari imeshuka daraja kufuatia kikosi hicho kumaliza nafasi ya 15 na pointi 27 katika Ligi Kuu kwa msimu wa 2025-2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shaibu amesema amefikia uamuzi wa kutoendelea na Mtibwa Sugar kwa msimu ujao wa 2026-2027 na sasa kuna baadhi ya klabu anaendelea kufanya nazo mazungumzo, japo bado hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa hadi sasa.

“Kuna baadhi ya klabu mbalimbali nimekuwa nazo katika mazungumzo na moja kati ya hizo tutakapofikia makubaliano nitaweka wazi, kwa sasa mashabiki zangu watambue nimeshaondoka Mtibwa Sugar na ninatafuta tena changamoto mpya,” amesema Shaibu.

Mwanaspoti linatambua, mshambuliaji huyo aliyejiunga na Mtibwa Sugar, Agosti 7, 2025, akitokea TMA FC ya jijini Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship, amejiunga na TRA United kwa ajili ya kuiongezea nguvu katika eneo la ushambuliaji.

Nyota huyo alijiunga na TMA msimu wa 2024-2025, akitokea KenGold aliyoipandisha Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, kisha kushuka msimu wa 2024-2025 na kuifungia mabao tisa ya Championship, huku akiwahi kucheza pia maafande wa Green Warriors.

Kwa msimu wa 2025-2026, katika Ligi Kuu Bara akiwa na Mtibwa Sugar, alihusika na mabao matatu kati ya 25 yaliyofungwa na kikosi hicho kizima, baada ya mshambuliaji huyo kufunga mawili na kuchangia bao lingine moja kwa maana ya kutoa asisti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *