Mbeya. Kwa watu wengi, oili chafu ni taka isiyo na thamani. Kwa kijana Ophurine Mwakipesile (50), imekuwa mali na fursa ya kumwingizia kipato kufuatia kuongeza thamani kupitia ubunifu wa kutengeneza majiko ya kupikia.

Mwakipesile ni mkazi wa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi, Wilaya ya Mbeya, ambaye amekuwa mashuhuri katika eneo hilo kwa kazi ya kutengeneza majiko hayo, huku akilenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Shughuli zake anazifanyia eneo lililo hatua kadhaa kutoka Barabara Kuu ya Tanzania-Zambia (TANZAM), ambako lipo chimbo lake la kujitafutia riziki ya kila siku.

Mwakipesile anasema hutumia vifaa mbalimbali, ikiwemo dumu la lita 20 la kuhifadhia oili chafu na feni ya kusukuma hewa baada ya kuwasha jiko kwa ajili ya matumizi ya kupikia.

Ukimkuta Mwakipesile, ni kijana mwenye bashasha anayefanya kazi bila kuchoka. Kila jiko analolitengeneza ni ushahidi wa safari yake ya kupambana na changamoto za maisha.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwakipesile anasema hakuwahi kusomea darasani ubunifu huo, lakini alijifunza miaka kadhaa iliyopita akiwa Arusha alikokwenda kutafuta maisha.

“Nilijifunza kwa rafiki yangu mmoja Arusha. Niliporudi Mbeya maisha yakawa magumu huku nikiwa na jukumu la kuwalea watoto wanne. Nikagundua kuwa njia pekee ya kusonga mbele ni kutumia ujuzi huu kujitafutia kipato,” anasema.

Anasema mwanzo haukuwa rahisi. Alikosa uzoefu wa kutosha na mara kadhaa alishindwa kupata matokeo aliyoyatarajia. Hata hivyo, hakukata tamaa.

“Nilikaa nikatafakari namna ya kuitunza familia yangu. Ugumu wa maisha ndio ulionipa ujasiri wa kuendelea kujaribu hadi nilipofanikiwa,” anasema.

Kiasi cha mtaji

Mwakipesile anasema mradi huo unahitaji mtaji wa kati ya Sh500,000 hadi milioni moja, lakini kutokana na mazingira magumu aliyokuwa nayo, alilazimika kuanza na Sh30,000 hadi Sh40,000 kwa kununua vifaa huku akikusanya oili chafu kutoka kwenye gereji zinazobadilisha mafuta ya magari.

“Ukitaka kutoboa usione aibu. Nilikuwa kama chizi, mimi na madumu na ndoo, nikisaka oili chafu kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Mbalizi na nje kwa lengo la kutimiza ndoto yangu ya kuwasomesha watoto wangu ili waje kuwa msaada wa baadaye,” anasema.

Hatua ya kwanza

Mwakipesile anasema kwa mtaji uleule, jiko la kwanza alilolitengeneza liliuzwa kwa Sh100,000. Fedha hizo zilimpa moyo wa kutengeneza mengine ya plati mbili, ambayo aliyauza kwa Sh200,000.

Anasema tangu aanze mradi huo ni miezi minne sasa, huku akijivunia kuwa soko limeongezeka na sasa hupokea oda mbalimbali kutoka kwa mama lishe, baba lishe na familia mbalimbali.

“Sasa ni miezi minne nafanya shughuli hii. Kimsingi sijutii, bali bado kilio changu ni mtaji ili kufikia malengo ya kupanua wigo wa uzalishaji kulingana na mahitaji ya soko,” anasema.

Changamoto

Anasema changamoto kubwa ni mtaji mdogo unaoshindwa kukidhi mahitaji ya wateja ndani na nje ya mkoa.

Nyingine ni pamoja na baadhi ya wateja kuweka oda, lakini kushindwa kuzichukua kwa sababu zisizo na mashiko au kubadilisha uamuzi wanapoona bidhaa za wateja wengine.

Mfumo wa jiko

Mwakipesile anasema matumizi ya majiko hayo ni rahisi kwa biashara na majumbani kutokana na teknolojia inayomruhusu mtumiaji kutumia mfumo salama usio na athari kwa mazingira na afya.

“Haya majiko yana mfumo wa kiteknolojia. Nafunga sehemu ya kudondosha matone ya oili chafu taratibu wakati wa kuwasha. Pia kuna feni ya kusukuma hewa inayosaidia kuongeza nguvu ya moto. Mfumo huo hauna moshi na hurahisisha kupika kwa muda mfupi.

Matumizi ya mteja

“Dumu moja la lita 20 linaweza kutumika kwa mwezi mmoja hadi miwili, kutegemeana na matumizi ya mteja. Mfumo wetu unadondosha matone kidogo kidogo, hivyo matumizi ya oili yanakuwa madogo,” anasema.

Mwakipesile anasema ili Tanzania ifikie malengo ya matumizi ya nishati safi, ni wakati sasa Serikali kuwawezesha vijana wabunifu kupata ujuzi zaidi ili kuisaidia jamii kuachana na matumizi ya nishati chafu ya mkaa na kuni.

“Ninaamini ubunifu unaweza kutatua changamoto mbili kwa wakati mmoja; kuleta ajira na kulinda mazingira. Ndiyo sababu naendelea kuboresha teknolojia hii na ningependa kuona vijana wengi zaidi wakijikita kwenye ubunifu,” anasema.

Katika hatua nyingine, Mwakipesile anasema ili aweze kufikia malengo yake anaomba Serikali na wadau wamshike mkono ili aongeze ubunifu zaidi na kutoa elimu pamoja na ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Kauli za wananchi

Mama lishe Jane Amos katika eneo la Mapelele amesema matumizi ya majiko hayo yamekuwa msaada mkubwa na yamepunguza gharama za matumizi ya nishati ya mkaa.

“Mimi nimetumia kwa mwezi mmoja sasa. Matumizi yake ni rahisi mno na unaweza kutumia kupikia maharage na kuiva kwa haraka tofauti na nishati ya gesi na mkaa, ambazo tunatumia kwa gharama kubwa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *