DODOMA. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amezitaka wizara na taasisi zinazonufaika na fedha za NBC Marathon zihakikishe zinatumika kwa uwazi na kwa kuzingatia thamani ya fedha, ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kuleta matokeo, tena matokeo yanayopimika.
Amesisitiza kuwa kila shilingi inayowekezwa katika mbio hizo zinapaswa kuleta matokeo yanayoonekana, kwa sababu unaposhughulika na masuala ya afya, unaongelea uhai wa Watanzania.
Aidha Waziri Mkuu amesema kuwa NBC Dodoma Marathon imeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya riadha kwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuhamasisha afya, kuimarisha ustawi wa jamii na kuchangia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kuboresha huduma za afya nchini.

Dk Nchemba amesema hayo leo Julai 26, 2026, alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa msimu wa saba wa NBC Dodoma Marathon uliofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ukiwa na kaulimbiu ya #KataWeseOkoaMaisha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu aliwapongeza Benki ya NBC, wadhamini na washiriki wote kwa kufanikisha tukio hilo na kusema serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuboresha afya na ustawi wa Watanzania.
“Napenda kuwapongeza waandaaji wa NBC, wadhamini na washiriki wote. Hili ni jambo jema; si la michezo pekee bali ni jukwaa la kufadhili na kuimarisha ustawi wa jamii,” alisema.

Alisema serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya na kuimarisha huduma za matibabu kwa kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Afya ni msingi wa maendeleo. Ukiwa na afya njema unaweza kushiriki shughuli za uzalishaji na hata mashindano kama haya ya marathon. Serikali itaendelea kuhakikisha jitihada hizi zinakuwa endelevu,” alisisitiza.