USHINDI wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa watetezi Kombe la Kagame, Singida Black Stars, haujampa utulivu kocha wa Jamus SC ya Sudan Kusini, Saber Ben Jabria raia wa Tunisia ambaye hesabu zake zimehamia kwa Simba SC, akiamini ndiyo wapinzani watakaowapa kazi ngumu zaidi katika Kundi B la CECAFA Kagame Cup 2026.
Jamus wanaoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, waliandika historia kwa kuwashangaza mabingwa hao watetezi kupitia mabao ya Laurent Ramazani na Mario Taban Cherelino katika mchezo uliochezwa Jumamosi Julai 25, 2026 kwenye Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda.
Ushindi huo umeiweka Jamus kileleni mwa kundi B, lakini Jabria amesema bado hakuna nafasi ya kusherehekea kwani wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Simba, timu anayoiheshimu kutokana na uzoefu wake mkubwa katika mashindano ya kimataifa.
Kocha huyo amesema ushindi dhidi ya Singida umewaongezea kujiamini, lakini anaamini watakutana na changamoto tofauti watakapocheza na Wekundu wa Msimbazi.
Mtunisia huyo akaongeza kuwa Simba ni timu yenye hadhi kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na mashindano ya CAF, jambo linalowafanya wajipange kwa umakini zaidi.
“Nina heshima kwa Simba kwa sababu ni timu yenye uzoefu katika mashindano ya Afrika na naamini ndiyo itakayotupa changamoto. Tutalazimika kucheza kwa kiwango cha juu zaidi kama tunataka kupata matokeo mazuri,” amesema.
Kauli hiyo imeongeza uzito wa mchezo wa kesho, Jumanne ambapo Simba na Jamus zitavaana katika mchezo unaoweza kuamua mwelekeo wa Kundi B huku Simba wakisaka ushindi wao wa kwanza baada ya suluhu dhidi ya Mogadishu City.
Kwa upande wa Singida Black Stars, watakuwa na kibarua cha kujinasua dhidi ya Mogadishu City.