
Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) imeonya kuwa mvua za El Nino zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu, huenda zikasababisha hasara ya zaidi Dola Bilioni 10 hadi 20 kwa mataifa ya Afrika.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Mkurugenzi wa maswala ya mazingira wa benki ya maendeleo ya Afrika, Anthony Nyong, amesema mvua hizo zinaweza kupunguza ukuaji wa uchumi wa nchi zilizoathirika hadi kufikia asilimia 1 hadi 2, huku pia ikisababisha uhaba wa chakula na maji, kuharibu miundombinu na kuongeza idadi ya watu wanaolazimika kuhama makazi yao.
Wataalamu wa hali ya hewa wameonya kuwa ongezeko la joto katika bahari ya Pasifiki linaweza kufanya El Nino ya mwaka huu kuwa miongoni mwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa, na kusababisha ukame, mafuriko na dhoruba katika maeneo mbalimbali ya Afrika.
Kati ya mwaka 2023 na 2024, El Nino ilisababisha ukame mkubwa Kusini mwa Afrika na mafuriko makubwa eneo la Afrika Mashariki, hali iliyochangia kupungua kwa uzalishaji wa mazao, kupanda kwa bei za vyakula na kuongezeka kwa kiwango cha maji ya bahari katika maeneo ya pwani.