
Dar es Salaam. Mbunge wa Suna Mashariki nchini Kenya, Junet Mohammed, amedai kuwa baadhi ya wabunge na maseneta walipokea fedha wakati wa mchakato wa kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, mwaka 2024.
Junet alitoa kauli hiyo jana, Jumapili, Julai 26, 2026, katika mkutano wa pamoja wa vyama vya United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) uliofanyika Kakamega.
Mbunge huyo alidai kuwa fedha zilitolewa kwa baadhi ya wabunge na maseneta kabla ya kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kumuondoa Gachagua madarakani.
Akizungumza katika mkutano huo, Junet alimtaja Seneta wa Kericho, Aaron Cheruiyot, akidai ndiye aliyekuwa msimamizi wa fedha hizo.
“Wakati tulikuwa tunamfukuza Gachagua kazi, kuna kitu kilitembea hapo bungeni. Accounting officer alikuwa Aaron Cheruiyot,” alisema.
Mbali na madai hayo, Junet aliwashutumu baadhi ya wabunge kwa kutumia vibaya fedha walizodaiwa kupokea, akisema walipaswa kuziwekeza katika miradi ya maendeleo, kama kujenga nyumba, badala ya kuzitumia kwa matumizi ya muda mfupi.
Gachagua aliondolewa madarakani Oktoba 2024 baada ya Bunge la Kitaifa la Kenya kupitisha hoja ya kumfungulia mashtaka ya kikatiba yaliyohusisha tuhuma za kukiuka Katiba, kuchochea migawanyiko ya kikabila, kudhoofisha mamlaka ya Serikali na kutoa kauli zilizodaiwa kwenda kinyume na misingi ya uongozi wa kitaifa.
Hata hivyo, baadaye Seneti ilipitisha uamuzi wa kumuondoa madarakani, hatua iliyomfanya kuwa Naibu Rais wa kwanza nchini Kenya kuondolewa madarakani kupitia mchakato wa mashtaka ya kikatiba tangu kuanzishwa kwa mfumo huo wa kikatiba. Kuondolewa kwa Gachagua kulikuja kutokana na kuzorota kwa uhusiano wake wa kisiasa na Rais William Ruto, huku tofauti zao zikionekana hadharani kwa miezi kadhaa kabla ya mchakato huo kuanza.
Baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, Rais Ruto alimteua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, kuwa Naibu Rais mpya.
Uteuzi wake uliidhinishwa na Bunge na, baadaye, akaapishwa kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Gachagua katika Serikali ya Kenya.