
Serikali ya Somalia imethibitisha kuwa wapiganaji saba wa kundi la kigaidi la Al-Shabab wanaofungamana na kundi la kigaidi la al-Qaeda wameuawa baada ya makabiliano ya saa kadhaa kufuatia shambulio kubwa dhidi ya gereza la Godka Jilow mjini Mogadishu, tukio ambalo ni miongoni mwa mashambulizi makubwa zaidi katika mji mkuu kwa miezi ya hivi karibuni.
Shambulio hilo lilianza Jumamosi kwa mlipuko wa bomu la gari, kisha kufuatiwa na milio mizito ya risasi na milipuko iliyosikika katika maeneo mbalimbali ya jiji. Serikali imesema wanajeshi watatu waliuawa katika makabiliano na magaidi.
Katika taarifa rasmi, Al-Shabab ilidai kuwa lengo la shambulio hilo lilikuwa kuwaokoa wanachama wao waliokuwa wakizuiliwa katika gereza hilo la chini ya ardhi, ambalo linajulikana kwa kuwahifadhi wapiganaji wa kundi hilo.
Afisa mmoja wa usalama aliyepo gerezani amenukuliwa na wanahabari akisema kuwa “mlipuko mkubwa ulisikika katika lango la seli, na mara moja milio ya risasi ikaanza.” Aliongeza kuwa vikosi vya ziada vilitumwa ili kuwamaliza wapiganaji hao.
Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa magaidi walitumia magari yaliyopakwa rangi kama yale ya shirika la ujasusi la taifa na walivaa sare zinazofanana na za jeshi la Somalia, hali iliyowaruhusu kupita kwa urahisi katika vizuizi vya ukaguzi vilivyolinda usalama wa mji mkuu. Wizara ya Usalama wa Ndani imeseema magari ya kijeshi hayakukaguliwa rasmi, jambo lililowezesha shambulio hilo.
Tukio hilo lilitokea saa chache tu baada ya serikali kufungua barabara kadhaa za Mogadishu kwa mara ya kwanza tangu zaidi ya miaka kumi, huku Waziri Mkuu Hamza Barre akieleza kuwa kuna “mabadiliko na maboresho yanayoonekana” katika hali ya usalama.
Gereza la Godka Jilow lipo karibu na ikulu ya rais, katika moja ya maeneo yanayolindwa zaidi mjini Mogadishu, jambo linaloibua maswali kuhusu madai ya maboresho ya usalama katika mji mkuu wa Somalia.
Tangu mwaka 2007, serikali ya shirikisho ya Somalia imekuwa ikipambana na kundi la Al-Shabab, ambalo linatajwa kuwa “kundi kubwa, tajiri zaidi, na hatari zaidi” miongoni mwa makundi yanayofungamana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda duniani, likidhibiti maeneo makubwa ya kusini na kati mwa Somalia.
Mji wa Mogadishu, ambao kihistoria umekuwa ukikumbwa na migogoro, unalindwa kwa nguvu kubwa ya kijeshi, ikiwemo vikosi vya Umoja wa Afrika na mtandao wa vizuizi vya ukaguzi vinavyofanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali ya jiji.